Junet ajitetea kufuatia matamshi yake "Baba akishinda serikali ni ya watu wa nyanza", adai yalitafsiriwa vibaya

Muhtasari

•Junet ambaye ndiye kiranja mkuu wa walio wachache bungeni alidai kwamba matamshi yalitafsiriwa na kuripotiwa vibaya.

•Alisema kuwa matamshi yake hayakumaanisha kuwa kuna jamii ambazo zitatengwa iwapo kinara wa ODM Raila Odinga atanyakua kiti cha urais.

•Alisema kwamba alishangaa alipoona namna watu walikosa kumuelewa huku akishtumu mrengo wa siasa wa Tangatanga.

JUNET.jfif
JUNET.jfif

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed hatimaye amejitokeza kujitetea kufuatia matamshi tatanishi ambayo alitoa siku ya Ijumaa.

Alipokuwa kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen usiku wa Jumatatu, mwandani huyo wa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga alisema kuwa watu walielewa matamshi yake isivyofaa.

Junet ambaye ndiye kiranja mkuu wa walio wachache bungeni alidai kwamba matamshi yalitafsiriwa na kuripotiwa vibaya.

"Yale ambayo nilisema Nyamira kwa siku mbili ambazo zimepita yamechukuliwa nje ya muktadha. Matamshi yangu yametafsiriwa, kuelekezwa na kuripotiwa vibaya" Junet alisema.

Mbunge huyo alisema kwamba alikuwa anaeleza jamii ya Abagusii inayopatikana katika eneo la Nyanza kwamba kwa sasa kuna nafasi ya mmoja wao kuongoza nchi ya Kenya.

Junet alisema kuwa matamshi yake hayakumaanisha kuwa kuna jamii ambazo zitatengwa iwapo kinara wa ODM Raila Odinga atanyakua kiti cha urais.

"Tulikuwa kwa hafla katika kaunti ya Nyamira ambapo jamii ya Gusii inapatikana. Kampeni hufanywa kienyeji. Nilikuwa nazungumzia watu wa pale, watu wa jamii ya Gusii. Niliwaambia kuwa kwa sasa sisi kama watu wa Nyanza tuko na nafasi ya kuongoza nchi. Kuna nafasi ya mmoja wetu kuongoza nchi. Sikumaanisha kwamba kuna yeyote atakayetengwa. Hiyo si kawaida yetu kama wakazi Nyanza" Alisema Junet.

Junet alisema kwamba alishangaa alipoona namna watu walikosa kumuelewa huku akishtumu mrengo wa siasa wa Tangatanga.

Alidai kwamba nia ya Tangatnga ni kueneza chuki dhidi ya Raila kwa kuwa wanahofia kuwa kinara wa ODM anaendelea kupata umaarufu mkubwa katika eneo la Mlima Kenya.

"Nilishangaa kuona namna watu wanaweza kuwa wameishiwa na matumaini haswa watu wa Tangatanga. Naona wamekosa mawazo. Sasa wanachukua kila kitu wapatacho ikutokana na ziara za Raila za hivi karibuni na jinsi amepokewa vizuri. Sasa wamerudi kueneza chuki dhidi ya Raila. Najua wameogopa kwa kuwa walidhani eneo la Mlima Kenya ni lao lakini Baba alipotembea pale mambo yalibadilika. Hawakuwa wanatarajia hayo" Junet alisema.

Mnamo siku ya Ijumaa alipokuwa anatoa hotuba yake kwenye hafla ya kuchanga pesa ambayo ilikuwa imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwemo Raila Odinga, waziri Fred Matiang'i na Mutahi Kagwe, Junet alisikika akidai kwamba iwapo  Raila Odinga atanyakua kiti cha Urais kwenye chaguzi kuu za mwaka ujao basi serikali itakuwa mikononi mwa watu wa Nyanza.

Junet alimuomba waziri wa afya Mutahi Kagwe  asikasirishwe na matamshi yake huku akidai kwamba eneo alilotoka la Mlima Kenya limekuwa likitawala kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.

"Hapa Nyanza sisi ni watu moja, sisi ni jamii moja. Tusiwe na wasiwasi. Baba akishinda, serikali ni yetu watu wa Nyanza, Sitaki watu wa gazeti wasikie hiyo, Mutahi Kagwe anaweza kasirika, lakini ata nyinyi mlikuwa nayo miaka ishirini na kadharika. Safari hii ni yetu watu wa Nyanza. Mutahi utakuja hapa kama mgeni" Junet alisema.

Matamshi ya mwanasiasa huyo hata hivyo hayajapokewa vyema haswa na wafuasi wa mpinzani mkubwa wa Raila Odinga, naibu rais William Ruto.