Ruto aahidi kupatia makahaba katika kaunti ya Makueni shilingi milioni moja

Muhtasari

•Ruto aliwaahidi kuwatumia angalau shilingi  milioni moja kwenye sacco ambazo wangeunda angalau wapate mtaji wa kufanikisha ndoto yao ya kufanya biashara yenye kuheshimika.

•Naibu rais aliendelea kupigia debe  mfumo wa kiuchumi wa bottom-up huku akisisitiza kwamba unaangazia kuinua maisha na wananchi wote haswa wenye kipato cha chini.

Image: FACEBOOK// WILLIAM SAMOEI RUTO

Naibu rais William Ruto ameahidi kupatia makahaba katika eneo la Mtito Andei shilingi milioni moja.

Alipokuwa anahutubia wakazi wa kaunti ya Makueni kwenye mkutano uliofanyika siku ya Jumatatu, mgombeaji huyo wa kiti cha urais mwaka ujao aliwahimiza makahaba waunde sacco ambapo angewatumia pesa zile.

Hapo awali makahaba hao walikuwa wametoa wito kwa naibu rais awapatie msaada wa pesa ambazo zingewasaidia kubadilisha kazi ili wajitose kwenye biashara zingine zenye kuheshimika.

Ruto aliwaahidi kuwatumia angalau shilingi  milioni moja kwenye sacco ambazo wangeunda angalau wapate mtaji wa kufanikisha ndoto yao ya kufanya biashara yenye kuheshimika.

Aliahidi kufuatilia na kuhakikisha kwamba makahaba wale wameanzisha biashara ya kuheshimika na kuona kuwa imestawi watakapopokea zile pesa.

Naibu rais aliendelea kupigia debe  mfumo wa kiuchumi wa bottom-up huku akisisitiza kwamba unaangazia kuinua maisha na wananchi wote haswa wenye kipato cha chini.

Ruto alisema kwamba mfumo wa bottom-up utawezesha wafanyibiashara wadogo na wakulima ambao kwa sasa wanagandamizwa na  wakopeshaji wanaodai faida kubwa.

Alisisitiza kuwa chama chake cha UDA ni cha kitaifa ambacho kitaleta pamoja Wakenya kutoka maeneo yote ya nchi bila ubaguzi.