Polisi 4 kushtakiwa kuhusiana na mauaji ya wanaume wawili Nairobi na Mombasa- IPOA

Muhtasari

•Uchunguzi wa IPOA umebaini kuwa konstabo sajenti Charles Mwakio, Koplo Julia Kimbiyo na Konstabo Peter Kananu wako na mashtaka ya kujibu kuhusiana na mauaji ya Leonard Muramba   ilhali Konstabo Lewis Nguyo Msuya anashtakiwa kwa mauaji ya Said Muktar Ibrahim.

•Konstabo Lewis Nguyo ambaye alikamatwa siku ya Ijumaa wiki iliyopita atakabiliwa na mashtaka ya mauaji.

Mahakama
Mahakama

Maafisa wanne wa polisi ambao wamehusishwa na mauaji ya watu wawili tofauti katika miji ya Nairobi na Mombasa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Uchunguzi wa IPOA umebaini kuwa konstabo sajenti Charles Mwakio, Koplo Julia Kimbiyo na Konstabo Peter Kananu wako na mashtaka ya kujibu kuhusiana na mauaji ya Leonard Muramba   ilhali Konstabo Lewis Nguyo Msuya anashtakiwa kwa mauaji ya Said Muktar Ibrahim.

Marehemu Muktar alipigwa risasi katika maeneo ya Korogocho, Nairobi mnamo November 12 mwaka wa 2017 ilhali Muramba alipigwa risasi katika maeneo ya Kisauni, Mombasa mnamo Agosti 15, 2013.

Kupitia kwa ripoti iliyochapishwa na IPOA siku ya Jumatano, sajenti Mwakio na Koplo Kimbiyo watashtakiwa kwa kosa la mauaji ya Muramba  bila kukusudia huku konstabo Peter Kananu akishtakiwa kwa kosa la kutelekeza kazi yake.

Kwa upande wa mauaji ya Ibrahim, konstabo Lewis Nguyo ambaye alikamatwa siku ya Ijumaa wiki iliyopita atakabiliwa na mashtaka ya mauaji.

Mnamo siku ya Jumatatu siku hii mahakama iliamuru Nguyo azuiliwe kwa kipindi cha siku kumi  ambapo atafanyiwa vipimo vya kiakili.

IPOA pia imependekeza polisi mwingine wa cheo cha ukonstabo akamatwe kuhusiana na mauaji ya Ibrahim.