Shule ya upili ya wasichana ya Buruburu yafungwa kufuatia mkasa wa moto huku uchunguzi uking'oa nanga

Muhtasari

•Usimamizi wa shule hiyo umetoa ilani  kwamba hatua kali itachukuliwa dhidi ya mwanafunzi yeyote atakayepatika kuhusika na tukio hilo.

•Hali ya afya ya wanafunzi 34 waliolazwa hospitalini ni imara ila mmoja wa wanafunzi ambao waliruka walipokuwa wanajaribu kuokoa maisha yao anaripotiwa kuvunjika mguu.

Bweni la shule la upili ya wasichana ya buruburu yateketea
Image: Hisani

Shule ya upili ya wasichana ya Buruburu imewaruhusu wanafunzi kuenda nyumbani kufuatia mkasa wa moto ambao uliteketeza bweni moja siku ya Jumapili.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kupatia nafasi uchunguzi wa kina kuhusiana na mkasa huo ambao ulitokea mwendo wa saa kumi unusu jioni kufanyika.

Usimamizi wa shule hiyo umetoa ilani  kwamba hatua kali itachukuliwa dhidi ya mwanafunzi yeyote atakayepatika kuhusika na tukio hilo.

Kwa sasa wanafunzi 35 wanaendelea kupokea matibabu, 19 kati yao wakitibiwa katika hospitali ya Metropolitan huku wengine 16 wakihudumiwa katika hospitali ya Jamaa.

Hali ya afya ya wanafunzi 34 waliolazwa hospitalini ni imara ila mmoja wa wanafunzi ambao waliruka walipokuwa wanajaribu kuokoa maisha yao anaripotiwa kuvunjika mguu.

Bodi ya shule hiyo imekutana na wazazi kuzungumzia tukio hilo ambalo liliibua hofu kote nchini jioni ya Jumapili.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya bweni la Kingdom shuleni humo kuteketea  katika hali tatanishi.

Mwalimu mkuu katika shule hiyo Bi. Caroline Maina alisema kuwa waliweza kuuthibiti moto ule kabla ya kuenea sana huku akieleza kuwa chumba kimoja tu katika bweni la Kingdom ndicho kilichoteketea.