(+Picha) Ajuza wa miaka 80 ataka kuwania kiti cha mwakilishi wa wanawake Nairobi kwa tikiti ya UDA

Muhtasari

•Bi Cecilia Mwangi almaarufu kama Shosh ambaye anamiliki duka la kuuza ala za sauti jijini Nairobi alipatana na katibu mkuu wa chama cha UDA, Veronica Maina siku ya Jumanne na kutangaza azma yake ya kuwania kiti cha mwakilishi wa wanawake.

Bi Cecilia Mwangi katika ofisi za UDA siku ya Jumanne
Bi Cecilia Mwangi katika ofisi za UDA siku ya Jumanne
Image: FACEBOOK// UNITED DEMOCRATIC ALLIANCE

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 80 anatazamia kumbandua Esther Passaris kutoka kwa kiti chake cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nairobi.

Bi Cecilia Mwangi almaarufu kama Shosh ambaye anamiliki duka la kuuza ala za sauti jijini Nairobi alipatana na katibu mkuu wa chama cha UDA, Veronica Maina siku ya Jumanne na kutangaza azma yake ya kuwania kiti cha mwakilishi wa wanawake.

Kupitia mtandao wa Facebook, chama cha UDA kinachohusishwa na naibu rais William Ruto kilitangaza kuwa Bi. Cecilia amejiunga rasmi na chama hicho na atakuwa katika kinyang'anyiro cha mwaka ujao.

"Cecilia Mwangi (Shosh)  80, ambaye ni mmiliki wa Shosh Sound Systems, ambaye alivuma kwenye vyombo vya habari vya kimataifa amekaribishwa UDA na katibu mkuu Generali Veronica Maina. Atawania kiti cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nairobi" UDA ilitangaza.

Mwanasiasa mwingine ambaye anamezea mate kiti hicho na tikiti ya UDA ni seneta wa kuteuliwa Millicent Omanga.

Omanga tayari ameanza kujipigia debe na kuboresha nafasi yake ya kumbandua Passaris wa chama cha ODM ambaye alinyakua kiti hicho mwaka wa 2017.