IEBC yawasilisha kesi mahakamani kupinga amri ya kuendeleza shughuli ya usajili wa wapiga kura

Muhtasari

•Hata hivyo shughuli ya kusajili wapiga kura itaendelea siku ya Jumatano huku mahakama ikisubiriwa kutatua kesi hiyo.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC ) imewasilisha kesi mahakamani kupinga amri ya mahakama ya kuendeleza shughuli ya usajili wa wapiga kura ambayo ilitolewa mapema wiki hii.

Siku ya Jumatatu mahakama kuu ya Eldoret ilizuia IEBC kusitisha shughuli ya usajili wa wapiga kura mnamo Novemba 2 kama ilivyokuwa imepangwa.

Mpiga kura Patrick Cherono pamoja na wakili wake Kairia Nabasenge walikuwa wamewasilisha kesi mahakamani wakilalamikia kuwa tume ya  IEBC haikuwa imeafikia lengo lake la kusajili wapiga kura wapya milioni 4.5.

Jaji Eric Ogolla aliamuru IEBC iendeleze shughuli hiyo hadi tarehe 9 Novemba ambapo kesi iliyowasilishwa na Cherono itasikizwa.

IEBC hata hivyo haikuridhishwa na uamuzi huo ikilalamika kuwa haijatengewa fedha za kutosha kuendeleza shughuli hiyo. 

Kesi iliyowasilishwa na IEBC siku ya Jumanne inatarajiwa kusikizwa asubuhi ya Jumatano. 

Hata hivyo shughuli ya kusajili wapiga kura itaendelea siku ya Jumatano huku mahakama ikisubiriwa kutatua kesi hiyo.