"Get a life and move on!" Lilian Ng'ang'a amwambia Mutua, asema gavana amekuwa akimtishia pamoja na walio karibu naye

Muhtasari

•Lilian ameweka wazi kwamba  hakuwa mke wala mpenzi wa Mutua ila walikuwa washirika wa muda mrefu tu.

•Lilian amesema kuwa gavana Mutua amemwagiza arejeshe pesa na mali yote ambayo aliwahi kumpatia walipokuwa pamoja.

Aliyekuwa mpenzi wa gavana Mutua Lilian Ng'ang'a
Aliyekuwa mpenzi wa gavana Mutua Lilian Ng'ang'a
Image: MERCY MUMO

Lilian Ng'ang'a amekanusha dhana kwamba yeye na aliyekuwa mpenzi wake gavana Alfred Mutua bado ni marafiki.

Kupitia taarifa kwa waandishi wa habari siku ya Alhamisi, Lilian alisema kuwa hakujakuwa na uhusiano mzuri kati yake na mwanasiasa huyo tangu mwezi Agosti.

Mpenzi huyo wa mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani ameweka wazi kuwa gavana Mutua alianza kumpatia vitisho tangu mwishoni mwa mwezi Agosti punde baada ya kuhudhuria sherehe yake ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa iliyofanyika katika hoteli ya Ole Sereni.

"Nilitamatisha uhusiano wangu na Alfred Mutua mwezi Juni mwakani. Mara kadhaa haswa wiki katika kipindi cha wiki mbili zilizopita  nimeona Mutua akisema kwa gazeti na mitandaoni kuwa sisi ni marafiki na eti uhusiano wetu ulitamatika kufuatia maafikiano ya pamoja. Huo ni uongo wake wa kawaida. Hatujazungumza naye tangu mwishoni mwa mwezi Agosti" Lilian amesema.

Lilian amedai kwamba  Mutua tayari  amepiga hatua ya kuchukua baadhi ya mali ambayo ilikuwa imeandikiishwa kwa jina lake. 

Amemshutumu gavana huyo kwa kuchukua na kuuza gari iliyokuwa imeandikishwa kwa jina lake na isitoshe akakabidhi dadake hisa za hoteli moja ambayo alikuwa amewekeza.

"Bwana Mutua ameguswa sana na kutengana kwetu. Ingawa nilisema nataka kusonga mbele na maisha yangu, alifikiria vingine" Lilian amesema

Lilian amedai kwamba Mutua ametishia kuchukua kila kitu anachomiliki na kumsababishia mahangaiko tele maishani.

Hali kadhalika amesema  kuwa gavana Mutua amemwagiza arejeshe pesa na mali yote ambayo aliwahi kumpatia walipokuwa pamoja.

"Mutua anatazamia kunidhulumu kisaikolojia na kiuchumi na lazima serikali imzuie!!" Alisema

Lilian amedai kuwa gavana huyo amekuwa akitishia kusababisha madhara kwa watu walio karibu naye ili kumuadhibu.

"Alisema kuwa kuna watu wamejitolea kuua watu walio karibu nami na akatishia kuwa huenda akakubali  ili apatie baadhi yao funzo. Kwa dharau alisema kuwa yeye ni mtu wa maana sana nchini na anaweza fanya chochote alichokuwa amepanga kunifanyia pamoja na marafiki wangu na asiadhibiwe. Alisema kuwa kuna watu ambao wako tayari na wamesubiri kunimaliza pamoja na marafiki wangu" Alisema.

Amesema kwamba mnamo Okotoba 7 alipiga hatua ya kuenda mahakamani kuomba agizo ya kumzuia mwanasiasa huyo kwa kuwa alihofia kwamba maisha yake yamo hatarini.

Lilian amesema kuwa Mutua amemshtumu kuwa mtumizi wa madawa ya kulevya huku akidai kwamba anatumiwa na wapinzani wake wa siasa kama gavana Kivutha Kibwana na Kalonzo Musyoka.

Ameomba Inspekta Jenerali wa polisi na DPP waingilie kati na waidhinishe kuharakishwa kwa uchunguzi  na kushtakiwa kwa Mutua kwa uhalifu ambao amemtendea.