Jamaa aliyeiba shilingi milioni 45 kutoka kwa akaunti za benki za wateja 481 akamatwa Narok

Muhtasari

•Nelson Kipkemoi (22) alikamatwa kutoka mafichoni yake eneo la Mulot, kaunti ya Narok baada ya kuhusishwa na genge la watapeli ambao wamekuwa wakikamua pesa kutoka kwa akaunti za Wakenya wasiojua

Pingu
Image: Radio Jambo

Jamaa mmoja anayeaminika kupanga na kufanikisha wizi wa zaidi ya milioni 45 kutoka kwa akaunti za benki za Wakenya anazuiliwa na wapelelezi baada ya kukamatwa alasiri ya Jumapili.

Nelson Kipkemoi (22) alikamatwa kutoka mafichoni yake eneo la Mulot, kaunti ya Narok baada ya kuhusishwa na genge la watapeli ambao wamekuwa wakikamua pesa kutoka kwa akaunti za Wakenya wasiojua.

Kulingana na DCI, Kipkemoi amekuwa akilenga akaunti zinazoendeshwa na benki moja kubwa nchini na kufikia sasa inadaiwa amefanikiwa kuiba pesa kutoka kwa akaunti za wateja 481 ambao wanatumia huduma ya 'Mobile Banking'.

Wapelelezi waliweza kumkamata mshukiwa na anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya Milimani siku ya Jumatatu ili kujibu mashtaka ya wizi yanayomkabili.