Wakili Hassan Nandwa apatikana ametupwa Mwingi

Muhtasari

• Hassan Nandwa alipatikana akiwa hai huko Mwingi siku ya Jumatatu saa moja asubuhi na baadaye kuunganishwa na familia yake.

• Haijabainika ni nani alikuwa nyuma ya kutekwa kwake na alikuwa wapi wakati huo.

Wakili Hassan Nandwa aliyepatikana akiwa hai baada ya kutekwa nyara kwa siku kadhaa
Wakili Hassan Nandwa aliyepatikana akiwa hai baada ya kutekwa nyara kwa siku kadhaa

Wakili aliyetoweka baada ya kutekwa nyara amepatikana ametupwa huko Mwingi.

Hassan Nandwa alipatikana akiwa hai huko Mwingi siku ya Jumatatu saa moja asubuhi na baadaye kuunganishwa na familia yake.

Hii ni baada ya kutoweka kwa zaidi ya wiki moja baada ya kutekwa nyara. Nandwa alitupwa takriban kilomita 200 kutoka Nairobi.

Haijabainika ni nani alikuwa nyuma ya kutekwa kwake na alikuwa wapi wakati huo. Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Hassan Ole Nado alisema amesikia kuhusu kuachiliwa kwa Nandwa lakini hakuwa na maelezo zaidi.

"Nimesikia amepatikana akiwa hai na ameunganishwa na familia yake lakini tunasubiri taarifa zaidi kuhusu tukio hili," alisema.

Msemaji wa Msikiti wa Jamia Abu Ayman alisema alikuwa amezungumza naye na familia yake na kwamba walikuwa Mwingi wakijitayarisha kwa safari ya kurejea Nairobi. "Ana afya njema.

Nimezungumza naye na yuko sawa na familia yake," alisema. Lakini mteja wake na mfungwa wa ugaidi Elgiva Bwire bado hajapatikana.

Muungano wa Wanasheria wa Kenya (LSK) ulikuwa umepanga maandamano ya nchi nzima kuhusu kutoweka kwa Nandwa na Elgiva. Wawili hao walitoweka tangu Oktoba 28 baada ya Bwire kuachiliwa kutoka jela.

Mawakili hao wanasema wanapanga kufanya maandamano ya amani kote nchini chini ya "Wiki ya Kampeni ya Utepe Zambarau", mnamo Jumatano Novemba 10, 2021.

 Nandwa alimwakilisha Elgiva, aliyekiri kuwa mfuasi wa kundi la kigaidi la al-shabaab na kuhusika katika shambulio la kigaidi la Oktoba 24, 2011 katika steji ya basi. 

 Elgiva ambaye pia anajulikana kwa jina la Seif Deen Mohamed almaarufu Japhar almaarufu Japhel Okuku almaarufu Abu Muadh hayupo baada ya kuachiliwa huru kutoka kwa Gereza la Kamiti Maximum.

Polisi walidai walipokea ripoti kwamba Elgiva aliwaahidi marafiki zake wa zamani ambao wanatumikia mashtaka mbalimbali ya ugaidi katika Gereza la Kamiti Maximum kwamba atafanya shambulio ili kuwaachilia huru mara tu baada ya kuachiliwa.