Gavana Mutua abwagwa chini katika awamu ya kwanza ya mzozo wake na Lilian Ng'ang'a

Kesi hiyo itatajwa Novemba 15 wakati ombi lake la kutaka kuzuiliwa kwa Mutua litakaposikizwa.

Muhtasari

• Mahakama ilitupilia mbali ombi la Mutua la kutaka kesi hiyo ihamishwe kutoka Nairobi hadi Machakos ambako alidai mzozo ulianza.

• Mutua alikuwa amedai kuwa mahakama ya Nairobi haina mamlaka ya eneo ya kusikiliza na kuamua kesi hiyo kwa msingi kwamba mzozo ulizuka ndani ya Kaunti ya Machakos.

Image: MERCY MUMO

Gavana Alfred Mutua amepoteza awamu ya kwanza ya kesi ya umiliki wa mali kati yake na mpenzi wake wa zamani Lilian Ng'ang'a.

Hii ni baada ya mahakama kutupilia mbali ombi la Mutua la kutaka kesi hiyo ihamishwe kutoka Nairobi hadi Machakos ambako alidai mzozo ulianza.

Siku ya Jumanne mahakama ilitupilia mbali ombi la Mutua na kuamuru kuwa kesi itaendlea jijini Nairobi.

Mutua alikuwa amedai kuwa mahakama ya Nairobi haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi hiyo kwa msingi kwamba mzozo ulianzia ndani ya Kaunti ya Machakos.

Mahakama hiyo pia ilitupilia mbali hoja ya gavana huyo  kwamba ilikosa mamlaka ya kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Ng'ang'a kwa misingi ya  thamani ya hisa zinazohusika.

Mutua pia alikuwa amedai kuwa masuala yaliyoibuliwa na Ng'ang'a katika kesi hiyo yalikuwa yameamuliwa katika korti nyingine  akiteta kuwa kuna kesi sawa na hiyo mbele ya mahakama ya kibiashara kati yao na mambo yaliyomo yanafanana kwa kiasi kikubwa.

Mutua pia alikuwa amedai kuwa mahakama haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua masuala hayo kwa sababu Lilian amekubali ndoa naye kwa hivyo mahakama haiwezi sikiza kesi inayohusu ugavi wa mali ya wanandoa.

"Maombi hayo ni ya kipuuzi, ya kukasirisha na ni matumizi mabaya ya mahakama. Yana dosari isiyoweza kurekebishwa na hayana mashiko," Mutua aliteta.

Mahakama ilitupilia mbali hoja zote sita za pingamizi za awali zilizotolewa na Mutua katika azma ya kutupilia mbali kesi ya Ng'ang'a.

Katika kesi hiyo, Ng'ang'a anaitaka mahakama kutoa maagizo ya kumzuia Mutua kwenda karibu na nyumba yake, mahali pa kazi au kuchukua mali yake yoyote huku wakisubiri kuamuliwa kwa mzozo wao.

Amedai kuwa Gavana huyo alihamisha hisa zake kwenye Ndash Enterprises kwa njia ya udanganyifu na kuzikabidhi dada yake bila idhini yake.

Lilian pia alisema Mutua alienda nyumbani kwake na kuchukua gari lake aina ya Toyota Harrier ambalo anapanga kuuza.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 15 wakati ombi lake la kutaka kuzuiliwa kwa Mutua litakaposikizwa.

(Utafsiri: Samuel Maina)