Hofu baada ya wapenzi wawili kupatikana wameuawa kinyama ndani ya nyumba Nairobi

Muhtasari

•Mwili wa mwanamke ulipatikana kwa choo ukiwa na majeraha mengi ya kisu kwenye matiti, bega na tumbo huku mikono yake ikiwa imefungwa nyuma kutumia kipande cha nguo.

•Mwili wa jamaa  ulikuwa na majeraha mengi ya kisu kwenye mgongo na shingo huku mikono yake pamoja na shingo zikiwa zimefungwa.

1513138
1513138

Wapelelezi wa maujai jijini Nairobi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na mauaji ya mwanaume mwenye umri wa miaka 18 pamoja na mpenzi wake ambao walipatikana wakiwa wameuawa  kinyama katika nyumba moja eneo la Umoja Zone 8, Kamukunji.

Maafisa wa DCI wameripoti kwamba miili ya vijana hao wawili ilipatikana baada ya babu ya marehemu kupiga ripoti kuwa mjukuu wake pamoja na mpenzi wake walikuwa wametoweka ghafla na kwa siku kadhaa simu zao hazikuwa zinajibiwa.

Awali kabla ya kuomba usaidizi wa polisi, mkongwe yule alikuwa amefika kwa marehemu kuangalia ikiwa alikuwa nyumbani ila akapata kukiwa kumefungwa huku  uvundo mkali  ukiwa unatoka mle ndani. Hapo akaelekea katika kituo cha Buruburu akaita polisi.

Polisi walipoingia walikumbwa na  damu iliyokuwa imetapakaa kila mahali na ishara za mapambano makubwa yaliyokuwa yameendelea mle ndani.

Mwili wa mwanamke ulipatikana kwa choo ukiwa na majeraha mengi ya kisu kwenye matiti, bega na tumbo huku mikono yake ikiwa imefungwa nyuma kutumia kipande cha nguo.

Polisi walipokuwa wanaendelea kuzunguka mle ndani walikumbana  na mwili wa pili ambao ulikuwa wa mjukuu wa mzee aliyepiga ripoti ukiwa umetupwa kwenye sakafu ya chumba cha malazi.

Mwili wa marehemu  ulikuwa na majeraha mengi ya kisu kwenye mgongo na shingo huku mikono yake pamoja na shingo zikiwa zimefungwa.

Baadhi ya vitu vya nyumba ikiwemo televisheni, vipakatalishi viwili, redio na simu za marehemu hazikuwepo

Wapelelezi walichunguza eneo la tukio na kuchukua ushahidi ambao ungewasaidia kutatua mauaji hayo tatanishi.