IEBC yaonya vyama vya kisiasa kuhusu sheria za uchaguzi

Muhtasari

• IEBC imeagiza vyama vya kisiasa kuwasilisha sheria zao zilizorekebishwa za uteuzi kama inavyotakikana chini ya Kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Uchaguzi. 

• Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema tume imebaini kuwa hakuna chama kati ya themanini na tisa ambacho kiliwasilisha kanuni zao za uteuzi ili kuhakikiwa Jumatatu.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeagiza vyama vyote vya kisiasa kuwasilisha sheria zao zilizorekebishwa za uteuzi kama inavyotakikana chini ya Kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Uchaguzi. 

Uwasilishaji wa sheria za uteuzi, kulingana na IEBC, unatarajiwa ndani ya siku kumi na nne na sio baada ya Jumanne Novemba 16, 2021 kutoka tarehe ambayo vyama vya kisiasa vilipokea mawasiliano kutoka kwa Tume ya kuviagiza kurekebisha sheria hizo. 

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, katika taarifa kwa vyombo vya habari, alisema tume imebaini kuwa hakuna chama chochote kati ya themanini na tisa ambacho kiliwasilisha kanuni zao za uteuzi ili kuhakikiwa Jumatatu Oktoba 18, 2021 ambacho kimeafikia matakwa ya sheria kikamilifu. 

"Vyama vya siasa vinajulishwa kuwa Tume itatoa cheti cha kuafikia sheria kuhusu kanuni za uteuzi zilizowekwa," alisema. Hata hivyo, Chebukati alitahadharisha kuwa kanuni za uteuzi ambazo hazizingatii kanuni zinazohitajika zitatupiliwa mbali. 

Alisema vyama vya siasa ambavyo havitatimiza matakwa haya havitapewa vyeti vya kufuata sheria hatua ambayo itavizuia kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa 2022. 

"Vyama vya kisiasa vinaweza kutafuta mwongozo wa kufuata sheria katika meza ya usaidizi wa kisheria katika tume hiyo kwenye ghorofa ya 7, Anniversary Towers," alishauri. 

IEBC hupitia sheria za uteuzi zilizowasilishwa na vyama vya kisiasa kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 27 (2A) cha Sheria ya Uchaguzi, 2011 na Kanuni ya 6 ya Uchaguzi (Mchujo wa Vyama na Orodha za Vyama), 2017.