Ruto akana kuwanyima chakula walinzi wake

Muhtasari

• Hii ilikuwa baada ya wizara ya mambo ya ndani kumwandikia naibu rais kuhusu mgao wa chakula wa maafisa wa usalama. 

• Kulingana na barua kutoka kwa wizara ya mambo ya ndani, Katibu wa kudumu Wilson Njenga alisema maafisa wa Ruto hawajapewa chakula. 

Naibu rais William Ruto akiandamana na walinzi wake katika makazi yake rasmi ya Karen
Naibu rais William Ruto akiandamana na walinzi wake katika makazi yake rasmi ya Karen

Naibu rais William Ruto amepuuzilia mbali madai kwamba maafisa wa polisi katika makazi yake ya kibinafsi na rasmi wanakufa njaa.

Akizungumza na gazeti la Nation, msaidizi wa Ruto David Mugonyi alisema wamewapa maafisa hao chakula cha kutosha.

"Malalamiko pekee ninayofahamu ni kucheleweshwa kulipwa kwa marupurupu yao. Maslahi yao yanashughulikiwa na Inspekta jenerali wa polisi," alisema. 

Hii ilikuwa baada ya wizara ya mambo ya ndani kumwandikia naibu rais kuhusu mgao wa chakula wa maafisa wa usalama. 

Kulingana na barua kutoka kwa wizara ya mambo ya ndani, Katibu wa kudumu Wilson Njenga alisema maafisa wa Ruto hawajapewa chakula. 

"Au kupewa marupurupu ya chakula ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vyema na kwa ufanisi," alisema. 

Njenga alisema maafisa hao wametumwa hapo kwa kazi za mchana/usiku na hawawezi kuondoka kutafuta chakula. 

"Hii ni tofauti na wenzao wa GSU ambao waliwabadilishwa na ambao walikuwa wakipata mgao wa chakula," alisema.

 "Madhumuni ya barua hii kwa hiyo ni kukuomba urejeshe mgao wa chakula kwa maafisa waliopelekwa kwa sasa katika makazi hayo mawili kwa ajili ya utoaji wa huduma bora." 

Barua hiyo ilitumwa kwa katibu mkuu wa utawala katika afisi ya naibu rais Abdul Mwaserah. 

Mwezi uliopita Ruto alichapisha picha kwenye Twitter akiwa na kikosi chake kipya cha ulinzi katika makazi yake rasmi mtaani Karen. 

Maafisa wa idara ya AP walichukua jukumu la kulinda makazi ya Ruto baada ya kuondolewa kwa vikosi vya GSU. 

Maafisa wa GSU pia waliondolewa nyumbani kwa Ruto kijijini Sugoi, mjini Eldoret, makazi yake ya Elgon View na makazi yake rasmi ya Karen jijini Nairobi. 

Ofisi ya IG iliita mabadiliko ya kawaida, lakini Mugonyi alisema serikali ilikuwa inahujumu usalama wa DP na kuyataja mabadiliko hayo 'ya kishetani'.