Uingereza yasitisha mpango wa kuajiri wauguzi kutoka Kenya

Muhtasari

• Uingereza kupitia idara yake ya Afya ilisema kwamba hakuna haja ya kuwasajili wauguzi zaidi kutoka Kenya ilihali kuna uhaba wa maafisa hao nchini Kenya.

• Hatua hiyo inaonekana kama pigo kwa maelfu ya wauguzi nchini Kenya ambao walitarajiwa kuhamia kazini nchini Uingereza.

Image: Getty Images

Serikali ya Uingereza imesitisha mpango wa kuwasajili wauguzi kutoka Kenya. Uingereza kupitia idara yake ya Afya ilisema kwamba hakuna haja ya kuwasajili wauguzi zaidi kutoka Kenya ilihali kuna uhaba wa maafisa hao nchini Kenya.

Hatahivyo wauguzi ambao walipata maombi ya kazi kutoka Uingereza hawataathiriwa na agizo hilo jipya.

Uingereza imeongeza kwamba itafanya uchunguzi zaidi kubaini ni kazi ngapi katika siku za usoni katika mpango wa ushirikiano wa mataifa hayo mawili utazifaidisha Kenya na Uingereza.

Hatua hiyo inaonekana kama pigo kwa maelfu ya wauguzi nchini Kenya ambao walitarajiwa kuhamia kazini nchini Uingereza.

Kenya na Uingereza zilifikia makubaliano kuhusu uhamiaji kwa lengo la kufanya kazi miongoni mwa wauguzi wa Kenya wakati rais Uhuru Kenyatta alipozuru nchini Uingereza mwezi Julai 2021.

Makubaliano hayo yalitiwa saini na waziri wa Afya nchini Uingereza Sajid Javid na mwenzake wa kazi nchini Kenya Simo Chelugui.

Chini ya makubaliano hayo , wauguzi wasio na ajira nchini Kenya walihitajika kuhudumu chini ya huduma ya afya nchini Uingereza ya NHS kabla ya kurudi Kenya.