Kaunti ya Nairobi yapata gavana mpya

Muhtasari

• Ann Kananu Mwenda ambaye amekuwa akihudumu kama naibu gavana wa Nairobi hatimaye ameapishwa kuwa gavana wa kaunti hiyo.

• Kananu anatarajiwa kuhudumu kama gavana hadi mwisho wa kipindi cha sasa mwaka 2022.

• Gavana huyo sasa anatarajiwa kuteua naibu gavana ambaye uteuzi wake kisha utaidhinishwa na bunge la kaunti. 

Ann Kananu Mwenda ambaye amekuwa akihudumu kama naibu gavana wa Nairobi hatimaye ameapishwa kuwa gavana wa kaunti hiyo.

Kananu anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa gavana Mike Sonko kufurushwa ofisini kupitia kura ya kutokuwa na imani naye katika bunge la kaunti ya Nairobi na kisha uamuzi huo kuidhinishwa na seneti.

Kananu ambaye ni mtaalam wa maswala ya uhalifu amekuwa akihudumu kama naibu gavana wa Nairobi tangu Januari mwaka 2021.

Kananu anatarajiwa kuhudumu kama gavana hadi mwisho wa kipindi cha sasa mwaka 2022.

Akitoa hotuba yake baada ya kuapishwa sikumya Jumanne Kananu alimpongeza rais Uhuru Kenyatta kwa uongozi wake bora na kinara wa ODM Raila Odinga kwa kuleta umoja katika kaunti ya Nairobi.

Kananu aliahidi kuendelea kushirikiana na NMS kuimarisha huduma kwa wakazi wa Nairobi.

Alisema kwamba yuko tayari na anauwezo kutekeleza majukumu ya gavana wa Nairobi kutumikia zaidi ya wakazi milioni sita wa Nairobi.

Gavana huyo sasa anatarajiwa kuteua naibu gavana ambaye uteuzi wake kisha utaidhinishwa na bunge la kaunti.