Ndugu ya gavana Joho kuwania kiti cha useneta kwa tikiti ya UDA

Muhtasari

•Siku ya Jumatatu Amir alijiunga na chama cha UDA kinachohusishwa na naibu rais William Ruto na kutangaza azma yake ya kuwania kiti cha seneta katika chaguzi za 2022.

Ndugu ya Joho Mohammed Amir apokewa UDA na Hassan Omar
Ndugu ya Joho Mohammed Amir apokewa UDA na Hassan Omar
Image: UNITED DEMOCRATIC ALLIANCE

Ndugu mkubwa wa gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, Mohammed Amir amejitosa kwenye siasa za kitaifa na anatumai kuingia seneti mwaka ujao

Siku ya Jumatatu Amir alijiunga na chama cha UDA kinachohusishwa na naibu rais William Ruto na kutangaza azma yake ya kuwania kiti cha seneta katika chaguzi za 2022.

Kupitia mitandao ya kijamii, UDA ilitangaza kwamba Amir alipokewa katika chama na aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar ambaye anamezea mate kiti  cha ugavana  baada ya kupoteza katika chaguzi za 2017.

"Kakake Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mohamed Amir, anajiunga na UDA kutangaza nia ya kuwania nafasi ya Seneti ya kaunti hiyo. Alipokelewa na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar" Ujumbe wa UDA ulisoma.

Hatua ya Amir ni ya kushangaza kuona kuwa ndugu yake, gavana  Joho ndiye naibu mwenyekiti wa chama pinzani cha ODM.

Amir anatumia kumbandua seneta wa sasa wa Mombasa Mohammed Faki ambaye anahudumu katika muhula wake wa kwanza.