Walinzi 7 wa gereza wakamatwa kufuatia kutoroka kwa wafungwa watatu wa kigaidi Kamiti

Muhtasari

•Waziri wa masuala ya ndani Fred Matiang'i alisema uchunguzi wa awali uliashiria kutoroka kwa wafungwa hao kulichangiwa sana na ulegevu na kuzembea kazini kwa walinzi.

•DCI imetoa ahadi ya shilingi milioni 60 kwa yeyote ambaye atatoa taarifa  kuhusu washukiwa hao wa ugaidi.

Pingu
Image: Radio Jambo

Walinzi saba katika  gereza ya Kamiti wamekamatwa kufuatia kutoroka kwa wafungwa watatu waliokuwa  wanahudumu kifungo kwa uhalifu unaohusiana na ugaidi.

Waziri wa masuala ya ndani Fred Matiang'i alisema uchunguzi wa awali uliashiria kutoroka kwa wafungwa hao kulichangiwa sana na ulegevu na kuzembea kazini kwa walinzi.

Alipokuwa anazungumza katika gereza ya Kamiti siku ya Jumatatu, Matiang' i aliapa kuhakikisha washukiwa zaidi wamekamatwa na kushtakiwa.

Pia alitangaza kuwa msako mkubwa unaohusisha maafisa maalum umeng'oa nanga.

Wafungwa ambao walitoroka ni pamoja na Musharraf Abdalla Akhulunga a.k.a Zarkarawi, Mohammed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo.

DCI imetoa ahadi ya shilingi milioni 60 kwa yeyote ambaye atatoa taarifa  kuhusu washukiwa hao wa ugaidi.

"Hatutaenda tu ambako uchunguzi utatuelekeza lakini tutachukua hatua thabiti kuhakikisha ulegevu wa aina hii hautokei tena kwa sababu unaweka watu wengi hatarini" Matiang'i alisema.

Matiang'i alisema serikali itawalinda watakaotoa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa wafungwa hao.

Inasemekana wafungwa ambao walitoroka wamejihami kwa silaha na ni hatari.

Matiang'i hata hivyo aliwasihi Wakenya wasiwe na wasiwasi kuhusu kutoroka kwa  wafungwa hatari ambako kumetoa hivi karibuni huku akihakikishia wananchi kuwa maafisa wa usalama wako machi na wameweza kuzuia mipango mingi ya mashambulizi ya kigaidi.

(Utafsiri: Samuel Maina)