Majambazi waliokuwa wamejihami wavamia baa Isiolo na kuiba pesa kisha kuacha watu na majeraha

Muhtasari

•Genge hilo linaripotiwa kupiga mlinzi risasi na kujeruhi watu wengine mle ndani kabla ya kuiba kiwango cha pesa kisichothibitishwa.

•Kutokana na hofu ya kutiwa pingu, mmoja wa majambazi wale alijaribu kupiga risasi lakini kabla hajalenga yeyote polisi mmoja alimpiga risasi na kumuua papo hapo.

crime scene 1
crime scene 1

Polisi katika kaunti ya Isiolo wanawinda genge la majambazi ambao walivamia baa ya 'Wazee Hukumbuka' iliyo mjini Isiolo usiku wa Jumanne.

Genge hilo linaripotiwa kupiga mlinzi risasi na kujeruhi watu wengine mle ndani kabla ya kuiba kiwango cha pesa kisichothibitishwa.

Kulingana na DCI, mwendo wa saa mbili usiku polisi walipokea simu kutoka kwa mmilki wa baa hiyo ambaye aliwafahamisha kuhusu uvamizi uliokuwa unaendelea.

Baada ya kupokea ripoti kuhusu uvamizi, polisi walifika katika eneo la tukio na kuziba milango yote kabla ya kutangaza kuwasili kwao na kuagiza majambazi wale wajisalimishe.

Kutokana na hofu ya kutiwa pingu, mmoja wa majambazi wale alijaribu kupiga risasi lakini kabla hajalenga yeyote polisi mmoja alimpiga risasi na kumuua papo hapo.

Jambazi mwingine kuona hivo alipiga risasi kiholela na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa watu waliokuwa wameenda kujiburusisha pale.

Zogo kubwa ilitokea pale na majambazi wakachukua fursa ile kukimbia na kutoweka.

Mwili wa jambazi aliyeuawa ulipelekwa katika mochari ya Nanyuki huku watu waliojeruhuwa wakipelekwa hospitali.

DCI Kinoti ametoa wito kwa yeyote aliye na taarifa kuhusu genge hilo apige ripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu.