Wakenya watakiwa kuwa waangalifu zaidi kufuatia milipuko miwili iliyotokea Uganda

Muhtasari

•Wakenya wanatakiwa kupiga ripoti wanapogundua tabia za kutiliwa shaka, miendo au vifurushi vilivyoachwa mahali pekee yake.

Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna

Serikali imehakikishia Wakenya kwamba usalama umeboreshwa katika maeneo yote ya nchi na kwenye mipaka kufuatia mashambulizi ya kigaidi ambayo yalitokea katika nchi jirani ya Uganda siku ya Jumanne.

Hata hivyo wananchi wamehimizwa kuwa waangalifu zaidi wanapokuwa kwenye maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na kuripoti matukio yoyote ya kutiliwa shaka.

Kupitia ujumbe ambao ulitolewa na msemaji wa serikali Cyrus Oguna siku ya Jumanne, Wakenya wanatakiwa kupiga ripoti wanapogundua tabia za kutiliwa shaka, miendo au vifurushi vilivyoachwa mahali pekee yake.

Oguna alisema kumekuwa na mipango mingi ya uhalifu ila maafisa wa usalama wameweza kuisitisha kwa wakati baada ya kupokea ripoti kuhusu matendo ya kutiliwa shaka.

"Tunachukua fursa hii kuwashukuru wakenya kwa ushirikiano wao na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa ambazo zimesababisha kukwamisha mipango mingi ya wahalifu na hivyo kuchangia kuimarisha usalama" Oguna alisema.

Amesema serikali ya Kenya imejitolea sana kuhakikisha kwamba raia wake wako salama kikamilifu.

Siku ya Jumanne, mwendo wa asubuhi milipuko miwili iliripotiwa katika mji mkuu wa nchi jirani ya Uganda, Kampala.

Ripoti zilionyesha kuwa mlipuko mmoja ulitokea kwenye jumba la maduka karibu na kituo cha Polisi cha Central na mwingine karibu na Bunge.

Majengo ya ofisi yalitikisika wakati milipuko hiyo ilipoanza, baadhi ya mashahidi walisema.

Kufuatia hayo usalama uliboreshwa zaidi jijini Nairobi huku maafisa wengi wa polisi wakionekana kushika doria katika maeneo mbalimbali ya jiji.