Jamaa afungwa miaka 2 kwa kuwa na pesa bandia

Muhtasari

• Mahakama ya Embu siku ya Jumatano ilimhukumu mwanamume mmoja kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Shilingi 50, 000 kwa kupatikana na pesa ghushi za Shilingi 11,000.

• Msako huo uliendelezwa hadi nyumbani kwake ambapo noti sita zaidi za 1, 000 ziligunduliwa na mtuhumiwa alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Manyatta.

Mahakama
Mahakama

 Mahakama ya Embu siku ya Jumatano ilimhukumu mwanamume mmoja kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Shilingi 50, 000 kwa kupatikana na pesa ghushi za Shilingi 11,000.

Hii ilikuwa baada ya Hakimu Mkazi Tony Kwambai kumpata Teddy Mutungi na hatia ya kosa la kuwa na noti bandia za Shilingi 1, 000 mnamo Julai 11, 2021 ndani ya Mji wa Manyatta huko Embu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mshtakiwa ambaye alikana kosa hilo na alikuwa nje kwa bondi alikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa rafiki yake ambaye alimlaghai katika biashara na noti bandia.

Afisa wa upelelezi, Richard Ruto aliambia mahakama kwamba walimkamata mshukiwa alipokuwa akipata kifungua kinywa katika hoteli moja mjini humo mwendo wa saa nne asubuhi na walipompiga msasa walimpata na noti ghushi za 1, 000 za jumla ya Shilingi 5,000.

Msako huo uliendelezwa hadi nyumbani kwake ambapo noti sita zaidi za 1, 000 ziligunduliwa na mtuhumiwa alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Manyatta.

Mutungi aliomba ahurumiwe akisema yeye ndiye pekee anayetegemewa na familia yake changa na pia alikuwa akimtunza mama yake mgonjwa.

Ombi lake hata hivyo likataliwa huku hakimu akisema kosa hilo lilitaka adhabu kali ili liwe funzo.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO