Jamaa akamatwa kwa kujaribu kutosheleza kiu chake cha mapenzi na nyanya yake wa miaka 86, Makueni

Muhtasari

•Mshukiwa alipompata nyanya yake kitandani alimshika shingoni na kufunga mdomo wake kabla ya kujaribu kujiburudisha naye.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Makueni wanazuilia jamaa mmoja aliyejaribu kubaka nyanya yake mwenye umri wa miaka 86.

Stephen Mutua Mutala (24) anaripotiwa kuvunja nyumba ya nyanyake iliyo katika eneo la Kalongo, Makueni mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Alhamisi na kunyemelea hadi kitandani.

Maafisa wa DCI wameripoti kwamba mshukiwa alipompata nyanya yake kitandani alimshika shingoni na kufunga mdomo wake kabla ya kujaribu kujiburudisha naye.

Baada ya ajuza yule kugundua kile ambacho mjukuu wake alikuwa anakusudia kufanya aling'ang'ana kadri ya uwezo wake na kwa neema zake Maulana akafanikiwa kupiga nduru na kuita usaidizi.

Jamaa kuona hivyo alichanganyikiwa akamgonga nyanyake kwenye mguu na kiti kisha kutimua mbio kuokoa maisha yake.

Majirani waliofika kujibu nduru za ajuza yule walimpata akilia kwa uchungu na akawasimulia kilichokuwa kimetendeka.

Wapelelezi walipopokea ripoti kuhusu kitendo hicho cha aibu walianzisha msako mkubwa na wakafanikiwa kumtia mshukiwa mbaroni na kumuweka kizuizini akisubiri kufikishwa mahakamani kijibu mashtaka ya jaribio la ubakaji yanayomkabili.