Wanafunzi walioshtakiwa kwa kuteketeza bweni waachiliwa kwa dhamana ya nusu milioni

Muhtasari

•Moto huo uliotokea Septemba 24, 2021, unakadiriwa kusababisha uharibifu wa mali ya Sh3milioni.

•Jaji aliwakumbusha wanafunzi hao kuwa watakabiliwa na adhabu kali iwapo watapatikana na hatia ili kuwa mfano kwa wanafunzi wengine wenye  nia ya kuchoma shule zao.

Mahakama
Mahakama

Wavulana wawili wa Shule ya Sekondari  ya Kisiriri wameachiliwa kwa bondi ya Sh500, 000 kila mmoja na Mahakama ya Narok baada ya kushtakiwa kwa kosa la kuchoma na kuharibu mali ya shule.

Wavulana hao  ambao walikamatwa Jumatatu na kuachiliwa kwa Bondi ya Polisi walishtakiwa kwa makosa mawili ya uchomaji na uharibifu wa mali katika Bweni la Mt Kenya katika shule hiyo.

Moto huo uliotokea Septemba 24, 2021, unakadiriwa kusababisha uharibifu wa mali ya Sh3milioni.

Hii ni licha ya upande wa mashtaka kupinga kuachiliwa kwao kwa dhamana, ikisema kuwa washtakiwa wanaweza kuharibu ushahidi kwa urahisi au wangekosa kuhudhuria kesi hiyo.

Hata hivyo, Hakimu Mkuu wa Narok, George Wakahiu, alisema washukiwa hao walikuwa wanafunzi wachanga ambao wanaweza kudhibitiwa kwa urahisi na usimamizi wa shule, kwa hivyo hawawezi kukosa kuhudhuria kesi mahakamani au kuchezea mashahidi.

"Katiba ya Kenya inatoa haki ya kumwachilia mshukiwa yeyote kwa masharti ya dhamana kwa sababu mtu hana hatia hadi atakapothibitishwa kuwa na hatia," Hakimu alisema.

Jaji Wakahiu aliwakumbusha wanafunzi hao kuwa watakabiliwa na adhabu kali iwapo watapatikana na hatia ili kuwa mfano kwa wanafunzi wengine wenye  nia ya kuchoma shule zao.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 22, 2021.

Katika muda wa miezi miwili iliyopita, makumi ya shule kote nchini zimechomwa kwa moto, na kuwalazimu wasimamizi wa shule kufunga shule kwa muda usiojulikana.

Hata hivyo, Serikali imeonya kuwa wanafunzi watakaokutwa na tukio la kuchomwa moto watafungiwa nje ya mfumo wa elimu na kwamba wazazi na wanafunzi watajenga upya shule zilizoathirika.

Wachanganuzi wanalaumu matumizi mabaya ya dawa za kulevya, mfadhaiko, wingi wa mtaala na uhusiano mbaya wa mzazi na mwanafunzi na mwalimu kwa mwelekeo uliokithiri wa machafuko shuleni.

(Utafsiri: Samuel Maina)