Watu 4 wafariki, 3 wajeruhiwa vibaya kufuatia ajali mbaya iliyohusisha magari manne Narok

Hali ya afya ya waliojeruhiwa ni imara kwa sasa.

Muhtasari

•Ajali hiyo ilitokea baada ya trela ambayo ilikuwa inapeleka majani chai Nairobi kupoteza mwelekeo ilipokuwa inateremka mlima na kugongana uso kwa uso na lori lingine iliyokuwa inaelekea Narok na kulipuka.

•Waliokuwa wamejeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya  kaunti ya Narok huku miili ya walioaga ikihifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.

Lori lashika moto baada ya ajali ya barabarani iliyohusisha magari manne katika eneo la Maltauro kaunti ya Narok Jumamosi jioni.
Lori lashika moto baada ya ajali ya barabarani iliyohusisha magari manne katika eneo la Maltauro kaunti ya Narok Jumamosi jioni.
Image: KIPLAGAT KIRUI

Habari na Kiplagat Kirui

Watu wanne walifariki na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya gari lao kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Maltauro, kaunti ya Narok usiku wa Jumamosi.

Ajali hiyo ambayo ilitokea katika barabara ya Narok - Mai Mahiu mwendo wa saa moja usiku ilihusisha magari manne.

Kulingana na shahidi, Benson Mutua, ajali hiyo ilitokea baada ya trela ambayo ilikuwa inapeleka majani chai Nairobi kupoteza mwelekeo ilipokuwa inateremka mlima na kugongana uso kwa uso na lori lingine iliyokuwa inaelekea Narok na kulipuka.

Magari mengine ambayo yalihusika kwenye ajali hiyo yalikuwa Pick-Up moja na Toyota Axio.

""Dereva wa trela hiyo alishindwa kulidhibiti baada ya kugonga bumps kabla ya kugonga lori na kufanya libingirike mara kadhaa na kushika moto muda mfupi baadaye," alisema shahidi.

Iliwachukua polisi na wakazi muda mrefu kufanikiwa kutenganisha magari hayo yaliyokuwa yameharibika na trela ili kufikia miili ya marehemu iliyokuwa imeharibiwa vibaya.

Waliokuwa wamejeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya  kaunti ya Narok huku miili ya walioaga ikihifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.

Inaripotiwa kuwa  hali ya afya ya waliojeruhiwa ni imara kwa sasa.

Magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo yalipelekwa katika kituo cha polisi cha Duka Moja.