Polisi wanachunguza kifo cha mfanyakazi wa BBC Nairobi

Muhtasari

• Kate Mitchell, raia wa Uingereza ambaye alikua akiifanyia kazi katika kitengo cha shirika la BBC Media Action katika baadhi ya mataifa ya Afrika alifariki siku ya Ijumaa.

• Bi Mitchel hivi karibuni aliifanyia kazi BBCMedia Action katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

• Maafisa wa polisi waliambia vyombo vya habari walikua wanakichunguza mauaji na kutafuta sababu zake.

Image: GETTY IMAGES

Maafisa wa polisi jijini Nairobi wameanzisha uchunguzi baada ya mfanyakazi wa BBC kupatikana amefariki jijini humo.

Kate Mitchell, raia wa Uingereza ambaye alikua akiifanyia kazi katika kitengo cha shirika la BBC Media Action katika baadhi ya mataifa ya Afrika alifariki siku ya Ijumaa.

Kitengo cha BBC Media Action ndio kinachohusika na uhisani wa idhaa hiyo na hutumia vyombo vya habari na mawasiliano kuangazia suala la ukosefu wa usawa duniani.

Haijulikani iwapo kifo cha bi Mitchell katika hoteli ambayo alikuwa akilala kina uhusiano na kazi yake katika shirika hilo la habari.

Na huku chanzo cha kifo chake kikiwa hakijulikani , maafisa wa polisi waliambia vyombo vya habari walikua wanakichunguza kama mauaji na kutafuta sababu zake.

''Mtu anayeshukiwa kuhusika na mauaji yake ..aliruka kutoka ghorofa ya nane ya hoteli hiyo kupitia dirishani baada ya kubaini kwamba walinzi wa hoteli hiyo walikuwa wanamfuata'', alisema kamanda wa jimbo la Nairobi Augustine Nthumbi akizungumza na wanahabari.

Bi Mitchel hivi karibuni aliifanyia kazi BBCMedia Action katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

''Sote tumeshangazwa na kutishwa na habari hizi mbaya'', alisema afisa mkuu mtendaji wa BBC Media Action Caroline Nursery katika taarifa.

"Kate alikuwa mfanyakazi aliyependwa sana ambaye alifanya kazi kama meneja mwandamizi wa miradi na amekuwa nasi kwa miaka 14. Alikuwa anajulikana sana katika shirika hili , hususana na wafanyakazi wetu Ethiopia , Sudan Kjusini , Zambia na London.

"Tunatuma rambirambi kwa familia yake na marafiki wake wengi duniani'' , aliongezea.