Serikali yaapa kutimiza ahadi ya Sh60M kwa waliosaidia kukamatwa tena kwa washukiwa wa kigaidi

Ni kweli raia walisaidia katika kukamatwa tena kwa washukiwa hao wa kigaidi.

Muhtasari

•Shioso ametoa hakikisho kwamba serikali inakusudia kutimiza ahadi yake itakapokamilisha kuthibitisha ambaye anastahili kuipokea.

•Polisi pia wamesema uchunguzi kuhusiana na kutoroka kwa wafungwa hao hatari ungali unaendelea vizuri huku kukiwa na ushahidi muhimu ambao umepatikana tayari.

Washukiwa watatu wa ugaidi walifika katika Gereza la Kamiti huku kukiwa na ulinzi mkali mnamo Novemba 18, 2021
Washukiwa watatu wa ugaidi walifika katika Gereza la Kamiti huku kukiwa na ulinzi mkali mnamo Novemba 18, 2021
Image: ANDREW KASUKU

Serikali hatimaye imevunja kimya kuhusu zawadi ya shilingi milioni sitini ambayo iliahidi kwa yeyote ambaye angetoa habari ambazo zingesaidia kukamatwa kwa wafungwa watatu  wa kigaidi ambao walitoroka katika gereza ya Kamiti mnamo Novemba 15.

Musharraf Abdalla, Joseph Juma na Mohammed Abdi walikamatwa  tena siku ya Alhamisi katika eneo la Mwingi, kaunti ya Kitui. Zawadi ya milioni 20 ilikuwa imewekwa kwa yeyote ambaye angesaidia kukamatwa kwa kila kila mmoja wa wafungwa hao.

Polisi kupitia kwa msemaji wao Bruno Isohi Shioso wamekiri kuwa raia walisaidia katika kukamatwa tena kwa washukiwa hao wa kigaidi.

"Kwa kweli kauli za watu kadhaa wanaodai kuhusika katika kukamatwa kwa washukiwa zimeripotiwa sana kwenye vyombo vya habari" Shioso alisema kupitia taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari Jumapili jioni.

Shioso ametoa hakikisho kwamba serikali inakusudia kutimiza ahadi yake itakapokamilisha kuthibitisha ambaye anastahili kuipokea.

Serikali hata hivyo imesema kutokana na hatari iliyopo huenda watakaopokea zawadi wakakosa kutangazwa hadharani ili kulinda usalama wao.

"Hali ya usalama ya tukio na hatari ya madhara kwa wale ambao kwa dhati walisaidia kukamatwa kwa washukiwa watatu wa thamani ya juu yaweza zuia ufichuzi kamili wa umma wa watakaopokea zawadi za pesa" Shioso amesema.

Polisi pia wamesema uchunguzi kuhusiana na kutoroka kwa wafungwa hao hatari ungali unaendelea vizuri huku kukiwa na ushahidi muhimu ambao umepatikana tayari.