Polisi apatikana akiwa amefariki ndani ya nyumba yake Kirinyaga

Mwili wake ulipatikana sakafuni bila majeraha yoyote.

Muhtasari

•Kulingana na kamanda wa polisi katika kaunti ya Kirinyaga Bernard Korir, afisa huyo Julius Mwangi Ndungu, 56, ambaye alihudumu kama OCS  alianguka na kufariki Jumatatu asubuhi.

Crime scene photo
Crime scene photo

Polisi katika kaunti ya Kirinyaga wanafanya uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo tatinishi cha afisa mkuu wa polisi aliyekuwa anahudumu katika kituo cha polisi cha Wang'uru eneo la Mwea Mashariki.

Kulingana na kamanda wa polisi katika kaunti ya Kirinyaga Bernard Korir, afisa huyo Julius Mwangi Ndungu, 56, ambaye alihudumu kama OCS  alianguka na kufariki Jumatatu asubuhi.

Kifo chake hata hivyo kiligunduliwa mwendo wa alasiri na maafisa wa polisi wengine.

 "Mmoja wa maafisa wadogo kituoni alienda kumuona katika makao yake rasmi mwendo wa saa kumi na moja alfajiri lakini mlango wa nyumba yake ulikuwa umefungwa kutoka ndani. Afisa huyo alibisha hodi mara nyingi, OCS hakujibu," Korir aliambia wanahabari.

Baada ya OCS huyo kukosekana kwa masaaa kadhaa maafisa walishuku kulikuwa na jambo na wakaandamana hadi kwake na kuvunja mlango ili waweze kuingia. Mwili wake ulipatikana sakafuni bila majeraha yoyote.

Alisema uchunguzi wa maiti utafanywa hivi karibuni  ili kubaini kilichosababisha kifo chake.

Alipoulizwa iwapo afisa huyo aliwahi kukabiliwa na tatizo lolote la afya wakati wa utumishi wake, bosi huyo mkuu alibaini kuwa hakufahamu.

Ndugu za marehemu waliarifiwa kuhusu kifo chake na mwili ukahamishwa hadi hospitali ya misheni ya Mwea.

(Utafsiri: Samuel Maina)