Sonko amgeukia mwanamke anayedai kumpa habari za kisiri

Muhtasari

•Merry Nkatha alienda katika kituo cha polisi cha Karen kutafuta ulinzi akisema anahofia maisha yake. Alisema anahofia Sonko au maajenti wake wanaweza kumdhuru kwa kukataa kushirikiana naye

• Katika chapisho refu la Facebook, Sonko alisema ana sauti na video 149 za mazungumzo yao ya mara kwa mara tangu Januari 2021.

• Amewasilisha malalamishi katika Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhusu majaji hao.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko amemgeukia mwanamke ambaye alitaka ulinzi wa polisi kutokana na vitisho vya gavana huyo wa zamani.

Merry Nkatha alienda katika kituo cha polisi cha Karen kutafuta ulinzi akisema anahofia maisha yake. Alisema anahofia Sonko au maajenti wake wanaweza kumdhuru kwa kukataa kushirikiana naye.

Alidai Sonko amekuwa akitaka kuwa shahidi wake katika kesi mbili dhidi ya Gavana Anne Kananu na Jaji Saidi Chitembwe miongoni mwa kesi zingine.

Lakini siku ya Jumanne, Sonko alidai kuwa ni Nkatha ambaye amekuwa akimpatia habari kwa muda wa miezi 10 iliyopita.

"Asichojua ni kwamba tumekuwa tukipata habari hizi kutoka kwake kwa miezi 10 iliyopita. Kwa sasa, sitaki kumhusisha zaidi kuhusiana na kutoa habari zinazohusishwa na kesi zote hizi ambazo zimeelezwa kwa ushahidi wa sauti na video,” alisema.

Katika chapisho refu la Facebook, Sonko alisema ana sauti na video 149 za mazungumzo yao ya mara kwa mara tangu Januari 2021.

Sonko alidai kuwa mazungumzo hayo yalijumuisha Shilingi milioni 315 alizolipwa wakili wake wa zamani ili kusambaratisha kesi ya kupinga kura ya kutokuwa na imani naye, kurudisha nyuma kesi hiyo, na hivyo kuwarai majaji wengine kwenye kesi hiyo kutoa uamuzi dhidi yake, pamoja na maelezo kuhusu matumizi ya ngono kuhujumu haki.

"Haya na maelezo mengine katika mfululizo wa sauti na video yametolewa kwa usahihi bila shaka yoyote," alisema.

"Kwa hivyo, ni wajibu wangu kwa watu wa Kenya kuangazia ukweli."

Sonko pia alitoa video akimshutumu Nkatha kwa kumlazimisha kufanya ngono.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO

"Kulingana na uthibitisho ufuatao katika simu ya video naye hivi majuzi, ni dhahiri kwamba madai yake ni feki," alisema.

Aliporekodi taarifa yake siku ya Jumatatu, Nkatha alidai alizuiwa na kutekwa nyara Jumamosi huko Karen na watu anaowafahamu ambao walimpigia simu Sonko na kujibu maswali ambayo yalikuwa tayari.

Sonko kisha akamrekodi. Alipewa chokoleti kula ambayo "ilikusudiwa kumtuliza". Mzungumzo hayo yameenea kwenye mitandao ya kijamii. Sonko alitoa sauti hiyo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii ambapo Nkatha anasikika akijibu maswali na kumhusisha Kananu na watu wengine. 

Sonko alikataa kutoa maoni yake kuhusu madai hayo Jumatatu. Kulingana na Nkatha, amemfahamu Sonko kwa takriban miaka miwili. Alisema yeye ni mwanabenki wa zamani na kwa sasa ni mpanga mikakati. 

Afisa mkuu wa polisi wa Langata Benjamin Mwanthi alisema wanachunguza madai ya utekaji nyara na kwamba mlalamishi atapata ulinzi wa serikali. Sonko amekuwa akitoa msururu wa sauti na video ambapo anawahusisha majaji wa mahakama kuu.

Amewasilisha malalamishi katika Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhusu majaji hao. Hapo awali, mawakili wa zamani wa Sonko walipata maagizo ya kumzuia kuendelea kuchapisha ufichuzi wowote dhidi yao kusubiri kusikizwa kwa kesi yao. 

Mawakili Cecil Miller na George Kithi Jumanne walipata maagizo ya kumzuia Sonko kuchapisha chochote kinachowahusu katika ufichuzi wake unaoendelea. Mahakama pia imemzuia kakake Jaji Said Chitembwe anayedaiwa kuwa Amana Said Jirani kuchapisha chochote kuhusu mawakili hao wawili.Jirani ameorodheshwa kama mshtakiwa wa pili pamoja na Sonko.