Sitakata tamaa! Miguna aapa kuendelea kushinikiza kurudi kwake Kenya

Muhtasari

•Mshauri huyo wa zamani wa kinara wa ODM Raila Odinga amesema kuendelea kwake kuzuiwa  kunaashiria kuwa nchi ya Kenya inaongozwa  na majambazi wahalifu ambao hawajali kuhusu sheria.

•Mwanasheria huyo amesema ukatili na ukandamizaji dhidi yake hautafanya apoteze matumaini katika kusonga mbele na vita vyake.

Miguna Miguna

Wakili na mwanasiasa maarufu Miguna Miguna ameendelea kukosoa kuzuiliwa kwake kurejea Kenya licha ya mahakama kumpa kibali cha kuchukua hati ya kumruhusu arejee nchini.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Miguna ameshtumu serikali ya Kenya kwa kukaidi amri ya mahakama na kukiuka haki zake.

Mshauri huyo wa zamani wa kinara wa ODM Raila Odinga amesema kuendelea kwake kuzuiwa  kunaashiria kuwa nchi ya Kenya inaongozwa  na majambazi wahalifu ambao hawajali kuhusu sheria.

"Sasa nimegundua bila shaka yoyote kwamba Kenya ni nchi iliyotekwa na majambazi wahalifu ambao hawajali amri za mahakama, utawala wa sheria, au katiba. Nimethibitisha kuwa ukiukaji wa haki zangu na kutotii amri za mahakama ni kuhusu kutokujali" Miguna amesema.

Miguna hata hivyo amesema licha ya masaibu ambayo yamemkumba ataendelea kupigania haki zake na kuhakikisha amefanikiwa kuingia nchini.

Mwanasheria huyo amesema ukatili na ukandamizaji dhidi yake hautafanya apoteze matumaini katika kusonga mbele na vita vyake.

"Hii hapa ni ahadi: Haijalishi wananifanyia nini. Haijalishi wanakuwa wakatili au wakandamizaji kiasi gani dhidi yangu. Haijalishi ni amri ngapi za mahakama wanazokaidi. Haijalishi watanilazimisha uhamishoni kwa muda gani. Lakini sitajikataa taamaa kamwe" Miguna amesema.

Miguna alitarajiwa kutua nchini Jumatatu wiki iliyopita .

Hata hivyo mwanasheria huyo hakuweza kufunga safari yake baada ya kampuni ya usafiri ya wa ndege 'Air France'  kumuonyesha barua ya tahadhari 'Red alert' kutoka Kenya jioni ya Jumatatu.

Kupitia ujumbe ambao alichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter, Miguna alifahamisha Wakenya kuwa alipatiwa taarifa kuhusu hali hiyo alipokuwa katika kituo cha ndege cha Berlin Brandenburg  nchini Ujerumani tayari kuabiri ndege ya kurejea hapa nchini.

"Hii ni kuwafahamisha Wakenya na ulimwengu mzima kwamba maafisa wa AirFrance katika kaunta ya kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Berlin Brandenburg wamenifahamisha punde tu kwamba Serikali ya Kenya iliwatumia "Red Alert" asubuhi ya leo kwamba hawawezi kunisafirisha hadi Nairobi. Bado nasubiri nakala" Miguna aliandika.

Siku ya Jumatatu mahakama ilimwagiza wakili Miguna Miguna achukue hati ya dharura ya usafiri kutoka kwa ubalozi wa Kenya jijini Ottawa, Kanada au Berlin Ujerumani.

Miguna hata hivyo hakuweza kuchukua hati hiyo na kufikia  sasa hajaweza kufunga safari yake kurudi nchini.