Mwaliko wa Raila kwa mkutano wa Wiper wakera wana Oka

Muhtasari

• Raila amekubali mwaliko huo, na kutuma ujumbe mzito wa kisiasa wa uwezekano wa makubaliano ya kisiasa na Kalonzo kabla ya uchaguzi wa urais wa 2022.

• Washirika wa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi wamemshutumu Kalonzo na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kwa kutuma ishara tofauti kuhusu kujitolea kwao kwa Oka.

• Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi pia wanaweza kuhudhuria baada ya wao kueleza nia ya kuungana na Oka. 

Image: Hisani

Muungano wa One Kenya Alliance una wasiwasi baada ya kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kumwalika kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa hafla muhimu ya chama chake katika ukumbi wa mazoezi wa Kasarani.

Washirika wa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi wamemshutumu Kalonzo na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kwa kutuma ishara tofauti kuhusu kujitolea kwao kwa Oka.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala aliambia gazeti la The Star kwamba atasusia Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa siku ya Alhamisi ikiwa Raila ataalikwa, na atawakusanya wafuasi wengine wa ANC kuususia mkutano huo.

"Ikiwa Muungano wa One Kenya ni tawi la timu ya Raila Odinga, basi tunapaswa kuvunja muungano huo na kutafuta marafiki wengine," Malala aliambia Star.

"Tunapaswa kuwa na ujasiri na ujasiri wa kutosha kuwaambia watu wetu kwamba hatuwezi kushikana na jambo bora ni kuachana. Tunapaswa basi kila mmoja kutafuta marafiki mahali pengine kwa sababu hatuwezi kutuma ishara tofauti kwa watu wetu."

Hata hivyo, aliyekuwa Mbunge wa Mwingi ya Kati Gideon Mulyungi, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati andalizi ya kpongamano la wajumbe la Wiper  alithibitisha kwa Star kuwa walialika "viongozi wa chama cha kitaifa, akiwemo Raila, pamoja na wageni wa kimataifa".

Raila amekubali mwaliko huo, na kutuma ujumbe mzito wa kisiasa wa uwezekano wa makubaliano ya kisiasa na Kalonzo kabla ya uchaguzi wa urais wa 2022.

"Ninaweza kuthibitisha kuwa kiongozi wa ODM amealikwa kwenye NDC kesho [Alhamisi] na bila shaka atahudhuria," katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema.

Katika mahojiano na gazeti la Star, Malala alisema kuwa mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi na wafuasi wake wamekuwa wakimfanyia kampeni Raila, jambo ambalo halikubaliki. “Juzi tu tulimwona Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Samuel Poghisio, akimpigia debe Raila kutwaa kiti cha urais.

Poghisio ni mshirika mkuu wa Gideon Moi, ambaye ni kinara wa Oka... Poghisio alisema waziwazi amekuwa akiwaambia viongozi wa Oka kwamba Raila ndiye chaguo bora...Je, mwanachama wa Kanu anawezaje kuwafanyia wapinzani wetu kampeni waziwazi?" Malala aliuliza. 

Raila alikosa kuhudhuria kongamano la Ford Kenya lakini akahudhuria lile la Gideon. Mkutano wa wajumbe wa ANC umepangwa kufanyika mapema mwaka ujao. Kalonzo pia amewaalika washirika wake wa Oka, wakiwemo Mudavadi, Gideon Moi, Moses Wetang'ula (Ford Kenya) na Cyrus Jirongo. 

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi pia wanaweza kuhudhuria baada ya wao kueleza nia ya kuungana na Oka. 

Takriban wajumbe 6,000 wanatarajiwa kujaza ukumbi wa Kasarani katika onyesho la kudhihirisha ushawishi wa kinara wa Wiper katika harakati za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta. 

Imeibuka pia kuwa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Wiper imefanya mabadiliko makubwa kwa uongozi wa chama ambayo yataidhinishwa katika NDC. 

Makamu huyo wa rais wa zamani anatarajiwa kupokea uthibitisho kutoka kwa wajumbe kutoka wadi zote 1,450 kote nchini kupeperusha bendera ya urais ya Wiper.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO