Afisa wa KDF ahukumiwa miaka 5 kwa kutoa barua gushi za usajili wa makurutu

Muhtasari

• Koplo Kiptum alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kupokea shilingi laki tatu kutoka kwa Charles Kipkorir mnamo Aprili 4 2021 akisingizia kwamba alikuwa na uwezo wa kumsajili mwanawe Brian Kipkemoi katika jeshi.

• Hakimu aliagiza kuwa hukumu yake itekelezwe kwa awamu na kumpa mtuhumiwa siku 14 kukata rufaa iwapo hakuridhika na uamuzi wa mahakama.

• Kiptum alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kutoa barua bandia ya kujiunga na jeshi kwa mlalamishi.

Wanachama wa Mahakama ya Kijeshi wakiwa katika kambi ya Lang’ata wakiongozwa na Kanali Lucas Teimuge na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Bernard Ochoi. Picha: KDF
Wanachama wa Mahakama ya Kijeshi wakiwa katika kambi ya Lang’ata wakiongozwa na Kanali Lucas Teimuge na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Bernard Ochoi. Picha: KDF

Afisa mmoja wa KDF siku ya Jumatatu alihukumiwa kifungo cha miaka mitano na nusu jela na Mahakama ya Kijeshi iliyokuwa na kikako katika kambi ya Lang’ata baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na makosa ya usajili wa makurutu.

Wanachama wa mahakama hiyo wakiongozwa na Kanali Lucas Teimuge na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Bernard Ochoi walimpata Koplo Fred Kiptum Kiplagat na hatia ya kujipatia pesa kwa njia ya ulaghai, kutoroka kazini na kutoa barua ghushi za usajili wa makurutu kujiunga na KDF.

Koplo Kiptum alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kupokea shilingi laki tatu kutoka kwa Charles Kipkorir mnamo Aprili 4 2021 akisingizia kwamba alikuwa na uwezo wa kumsajili mwanawe Brian Kipkemoi katika jeshi. Pia alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani kwa kupokea shilingi 102,500 kutoka kwa Brian Kipkemoi siku hiyo hiyo akisingizia kwamba alikuwa na uwezo wa kushawishi kuajiriwa kwake katika jeshi.

Zaidi ya hayo, Kiptum alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kutoa barua bandia ya kujiunga na jeshi kwa mlalamishi, kitendo ambacho alipaswa kujua ni kosa la jinai na kifungo cha miezi sita jela kwa kutoroka kazini kwa siku 90 bila ruhusa hadi alipokamatwa tarehe 3 Mei 2021.

Hakimu aliagiza kuwa hukumu yake itekelezwe kwa awamu na kumpa mtuhumiwa siku 14 kukata rufaa iwapo hakuridhika na uamuzi wa mahakama.