Dereva aliyefutwa baada ya kuripoti wanafunzi waliokuwa wanavuta bangi na kulewa apata kazi katika kaunti ya Nyeri

Muhtasari

•Gavana Mutahi Kahiga aliahidi kumwajiri Maina kama dereva katika idara moja ya serikali ya kaunti ya Nyeri.

•Kahiga alimpokea dereva huyo ofisini kwake ambako alimkabidhi cheti na kutumia fursa ile kulaani matumizi ya madawa ya kulevya miongoni mwa vijana.

John Maina Muthoni akabidhiwa cheti na gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri
John Maina Muthoni akabidhiwa cheti na gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri
Image: FACEBOOK// GOVERNOR MUTAHI KAHIGA

Je wamkumbuka dereva John Maina Muthoni ambaye alipoteza kazi yake masaa machache tu baada ya kuripoti wanafunzi waliokuwa wanavuta bangi na kubugia vileo ndani ya matatu aliyokuwa anaendesha?

Siku ya Jumanne, kaunti ya Nyeri imemsherehekea dereva huyo kwa ushujaa ambao alionyesha wakati alikatiza safari ya kupeleka wanafunzi aliokuwa amebeba jijini Nairobi na kuelekea moja kwa moja hadi kituo cha polisi kuripoti uhalifu waliokuwa wanatenda.

Gavana Mutahi Kahiga aliahidi kumwajiri Maina kama dereva katika idara moja ya serikali ya kaunti ya Nyeri.

"Ningependa kusherehekea John Maina Muthoni, dereva wa zamani wa 2NK, dereva shujaa ambaye aliripoti wanafunzi baada ya kugundua walikuwa wanavuta bangi na kukata maji. Serikali yangu itampatia kazi kama dereva katika idara yetu moja" gavana Kahiga alitangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Kahiga alimpokea dereva huyo ofisini kwake ambako alimkabidhi cheti na kutumia fursa ile kulaani matumizi ya madawa ya kulevya miongoni mwa vijana.

"Matumizi ya dawa za kulevya ni uhalifu ambao unavunja nyoyo za wazazi na kuharibu maisha ya wanaume na wanawake wadogo na tunalaani tabia hiyo kabisa" Alisema Kahiga.

Takriban wiki mbili zilizopita Maina alikuwa anaendesha matatu ya kampuni ya 2NK kutoka Karatina kuelekea Nairobi akisafirisha wanafunzi 14 wa shule ya Sekondari ya Fred Grammar waliokuwa wanaenda nyumbani kwa kipindi cha likizo fupi.

Walipofika eneo la Kibingoti, Maina aligundua wanafunzi aliokuwa amebeba walikuwa wanavuta bangi na kunywa pombe ndani ya gari.

Alijaribu kuwasihi wakome ila wakaanza kumtishia na kumuagiza aachane nao ashughulike na kuendesha gari tu na hapo ndipo akageuza safari na kuendesha hadi kituo cha polisi. Wanafunzi wale hata hivyo  walipogundua kilichokuwa kinaendelea waliruka kupitia madirisha kabla ya kuwasili kituoni.

Baadae Maina alitumia ukurasa wake wa Facebook kutangaza kwamba alifutwa kazi punde baada ya kupiga ripoti ile.

"Mimi kama dereva wa 2NK nimepoteza kazi yangu kwa sababu ya kuripoti wanafunzi waliokuwawanatumia bangi na pombe kwenyegari. Sasa wananinyanyasa" Maina alisema.

Hata hivyo kampuni ya 2NK ilijitokeza kupuuzilia mbali madai ya Maina ikisema alisimamishwa kazi kufuatia kesi ya kutokabidhi mwenye matatu mapato yake ya kila siku kama walivyokuwa wamekubaliana ambayo ilikuwa inamkabili.