Ndugu wawili washambuliwa kwa risasi wakitoka mahakamani Kiambu

Muhtasari

•Ndugu hao walikuwa wanatoka katika mahakama ya Gatundu baada ya kuhudhuria kesi ambayo wameshtakiwa kwa kuiba mazao ya shamba wakati walikumbuna na masaibu hayo.

•Wahasiriwa waliweza kunusurika kifo ila wakaachwa na majeraha mabaya kifuani, mikononi, kwenye miguu na mabega. 

Picha ya Bunduki
Picha ya Bunduki
Image: HISANI

Ndugu wawili wamelazwa katika hospitali moja kaunti ya Kiambu wakiwa hali mahututi baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana walipokuwa wanatoka mahakamani asubuhi ya Alhamisi.

Ndugu hao walikuwa wanatoka katika mahakama ya Gatundu baada ya kuhudhuria kesi ambayo wameshtakiwa kwa kuiba mazao ya shamba wakati walikumbuna na masaibu hayo.

Kulingana na DCI, tukio hilo lilitokea mwendo wa saa nne asubuhi  na kusababisha hali ya wasiwasi miongoni mwa wakazi.

Mashahidi walisema washambuliaji wawili waliokuwa wamejihami kwa bastola waliwasili nje ya  mahakama kwa pikipiki na kuanza kuwapiga ndugu wale risasi kisha kutoweka. Nambari ya usajili ya pikipiki ambayo washambuliaji walitumia ilikuwa imefichwa.

Wahasiriwa waliweza kunusurika kifo ila wakaachwa na majeraha mabaya kifuani, mikononi, kwenye miguu na mabega. 

Ndugu hao walikimbizwa hospitalini ambako wanaendelea kuhudumiwa huku msako wa washukiwa ukiong'oa nanga. 

Wapelelezi waliofika katika eneo la tukio waliweza kupata katriji  tano za risasi zilizokuwa zimetumika.