Gari la miraa lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi laua kondoo 165 Lamu

Barisa aliwaita polisi wamsaidie kusaka dereva yule ili apate kufidiwa kwa kondoo wake waliokufa.

Muhtasari

•Dereva wa gari hilo la miraa aliendelea na safari yake kwa kasi baada ya ajali na kumuacha Bapesa akihesabu hasara.

•Haya yanajiri wakati ambapo wafugaji huko Lamu wanaendelea kupoteza mamia ya mifugo wao kutokana na ukame.

Mizoga ya kondoo 165 waliogongwa na gari la miraa lililokuwa likienda kasi huko Lamu siku ya Ijumaa.
Mizoga ya kondoo 165 waliogongwa na gari la miraa lililokuwa likienda kasi huko Lamu siku ya Ijumaa.
Image: CHETI PRAXIDES

Mfugaji mmoja katika kaunti ya Lamu amepoteza kondoo 165 baada ya gari la Miraa lililokuwa linaenda kwa mwendo wa kasi kuwagonga siku ya Ijumaa.

Kondoo watano pekee ndio walinusurika katika tukio hilo lililotokea katika eneo la Gamba kwenye barabara ya Lamu-Garsen.

Mfugaji Barisa Bapesakutoka kijiji cha Bandi aliyekuwa amejawa na ghadhabu alisema kondoo wake walikuwa wanavuka barabara kuelekea malishoni wakati tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea.

Dereva wa gari hilo la miraa aliendelea na safari yake kwa kasi baada ya ajali na kumuacha Bapesa akihesabu hasara.

Inaaminika gari hilo lilikuwa linaelekea Lamu kupeleka MIraa iliyokuwa imetoka Meru.

Barisa aliwaita polisi wamsaidie kusaka dereva yule ili apate kufidiwa  kwa kondoo wake waliokufa.

"Ni uchungu kupoteza kondoo 165 kwa sababu mtu alikosa kumakinika. Dereva hakusimama nikashindwa kurekodi namba. Ninaomba polisi wanisaidie kumtambua na kupata haki,” Bapesa alisema.

“Dereva alipuuza tu alama za barabarani na kuwagonga kondoo wangu. Hii ndiyo riziki yangu. Sina kingine.”

Eneo ambalo ajali ilitokea ni sehemu inayojulikana kuwa kivuko cha wanyama katika barabara ya Lamu-Garsen na kuna alama za barabarani zinazoonekana zinazowahitaji madereva kupunguza mwendo kwa sababu ya idadi kubwa ya mifugoambao huvuka  ikiwemo ng'ombe, kondoo na mbuzi .

Haya yanajiri wakati ambapo wafugaji huko Lamu wanaendelea kupoteza mamia ya mifugo wao kutokana na ukame.

Wafugaji walikusanyika katika eneo la tukio na kufanya maandamano kudai haki kwa mwenye kondoo.

“Mkulima huyu anapaswa kulipwa fidia. Wenye magari wanapaswa kujua kwamba Minjila, Gamba, na Witu ni maeneo ya wafugaji na hivyo wanapaswa kutarajia makundi makubwa ya mifugo kuvuka barabara,” Kubow Mohamed alisema.

Kamishna wa kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alisema polisi walikuwa wanamsaka dereva wa miraa.

Aliwatahadharisha madereva wa magari haswa ya miraa wanaopita barabarani dhidi ya kuendesha gari kwa kukosa umakinifu.

“Nimepokea taarifa na uchunguzi unaendelea. Tunamfuatilia dereva na tutahakikisha haki inatendeka,” Macharia alisema.

(Utafsiri: Samuel Maina)