Alfred Mutua aahidi wanandoa wapya zawadi ya Sh500,000 hadi milioni akichaguliwa kuwa rais

Muhtasari

• Mutua alisema serikali yake itakabidhi wanandoa pesa zile kama mkopo mkopo wa kuanza maisha ambao utalipwa kwa kipindi cha miaka 20.

•Pia aliahidi kutengenezea vijana nafasi milioni tano mpya za ajira katika kipindi cha  miaka mitatu yake  kwanza uongozini.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua wakati wa uzinduzi wa manifesto yake ya Urais katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Desemba 5, 2021.
Gavana wa Machakos Alfred Mutua wakati wa uzinduzi wa manifesto yake ya Urais katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Desemba 5, 2021.
Image: ISAIAH LANGAT

Gavana wa Machakos Alfred Mutua ameahidi zawadi ya shilingi laki tano hadi shilingi milioni moja kwa kila wanandoa wapya iwapo atachaguliwa kuwa rais mwaka ujao.

Alipokuwa anazindua manifesto yake ya urais katika hoteli ya Panari jijini Nairobi siku ya Jumapili, Mutua alisema serikali yake itakabidhi wanandoa pesa zile kama mkopo mkopo wa kuanza maisha ambao utalipwa kwa kipindi cha miaka 20.

"Wanandoa wapya ambao wameoa hivi majuzi watapokea mtaji wa awali kutoka kwa serikali yangu wa shilingi nusu milioni hadi milioni moja kama mkopo ambao utalipwa kwa kipindi cha miaka 20  kwa kiwango cha riba cha 5.05%. kama zawadi kutoka kwa serikali yangu kuwekeza katika boma yao mpya na kuimarisha  taasisi ya ndoa" Mutua alisema.

Mutua alisema mkopo ule ungesaidia wanandoa pakubwa katika kuanza familia na hawatakuwa katika shinikizo ya kulipa haraka.

Mgombeaji huyo wa kiti cha urais mwaka ujao pia alikuwa na habari njema kwa vijana huku akiahidi kutengeneza nafasi milioni tano mpya za ajira katika kipindi cha  miaka mitatu yake  kwanza uongozini.

Mutua aliahidi kukuza sekta ya burudani ambayo kwa sasa imefurikwa zaidi na vijana ambao wanaitegemea kupata mapato ya kila siku.

“Serikali yangu itaunda ajira mpya milioni 5 kwa vijana katika miaka mitatu ya kwanza huku tasnia ya burudani ikiwa mzalishaji mkubwa wa mapato. Kutakuwa na vituo vya bure vya utayarishaji wa muziki na video katika kila kaunti ili kukuza talanta.” Mutua alisema

Mutua pia aliahidi kukuza uchumi mara dufu kila mwaka na kupigana vikali na ufisadi unaoangamiza uchumi wa nchi.