Jirani auawa kwa mshale akijaribu kutenganisha vita kati ya ndugu wawili Marakwet

Muhtasari

• Kemboi alichukua upinde na mshale wake na kumlenga kaka yake ila kwa bahati mbaya mshale ule akamkosa na kupata mguu wa jirani yao Edwin Kibor

•Wanakijiji waliojawa na ghadhabu baada ya kupokea habari kuhusu kifo cha Kibor waliteketeza  nyumba 12 na maghala 8 ya familia ya kina mshukiwa ambaye aliingia mitini baada ya tukio hilo

crime scene 1
crime scene 1
Image: HISANI

Mwanaume mmoja alipoteza maisha yake baada ya kupigwa kwa mshale alipojaribu kutenganisha vita kati ya ndugu wawili katika kijiji cha Kipchumwa, eneo la Marakwet Mashariki.

Kulingana na DCI, Joel Kitum na kaka yake mdogo Onesmus Kemboi walikuwa wanapimana nguvu kufuatia mzozo kuhusu deni la familia la ng'ombe mmoja wakati msiba huo ulitokea.

Inaripotiwa kwamba Kemboi alichukua upinde na mshale wake na kumlenga kaka yake ila kwa bahati mbaya mshale ule akamkosa na kupata mguu wa jirani yao Edwin Kibor.

Kufuatia hayo Kibor alikimbizwa katika hospitali ya misheni ya  Endo huku damu ikimtirirka tiriri. Kwa bahati mbaya mhasiriwa alipokuwa anahudumiwa aliangamia kutokana na jeraha mbaya ambalo alikuwa amepata.

Wanakijiji waliojawa na ghadhabu baada ya kupokea habari kuhusu kifo cha Kibor waliteketeza  nyumba 12 na maghala 8 ya familia ya kina mshukiwa ambaye aliingia mitini baada ya tukio hilo.

Wazee wa kijiji walikutana na kuthibiti hali ili kuzuia kuharibiwa kwa mali zaidi huku msako wa mshukiwa uking'oa nanga.