Kijana na mwalimu mkuu wajitia kitanzi Narok

Muhtasari

•Mwili wa mvulana mwenye umri wa miaka 19 ulipatikana ukining'inia kutoka chumbani kwake asubuhi ya leo.(Jumatatu)

•Mwili wa Olonana, 34, haukuwa na majeraha yaliyoonekana lakini marehemu alikuwa ameacha barua ya kujitoa mhanga akiwaomba walimu wenzake na familia kumsamehe kwa hatua aliyochukua.

meru
meru

Mvulana mmoja na naibu mwalimu mkuu walijitoa uhai katika visa viwili tofauti katika Kaunti Ndogo ya Narok Kaskazini.

Kulingana na ripoti ya polisi, kisa cha kwanza kilitokea katika shamba la Father Daiyia, karibu na mji wa Narok ambapo mwili wa mvulana mwenye umri wa miaka 19 ulipatikana ukining'inia kutoka chumbani kwake asubuhi ya leo.(Jumatatu)

“Polisi walipokea taarifa kutoka kwa babake mvulana huyo ambaye aliarifu kuhusu kifo cha mwanawe. Walipozuru eneo la tukio,  walipata mwili huo ukining’inia kutoka darini huku kitambaa kikiwa kimefungwa shingoni,” alisema kamanda wa polisi wa Narok Kizito Mutoro na kuongeza kuwa mwili huo haukuwa na majeraha yanayoonekana na hakuna barua ya kujitoa mhanga iliyopatikana.

Wakazi wa shamba la Father Daiyia waliomboleza marehemu, wakimtaja kuwa mvulana mtulivu ambaye alishirikiana vyema na umma.

“Habari za kifo chake zilishangaza sana, nilimfahamu mvulana huyo tangu akiwa mdogo kwa sababu alipenda ushirika wa watoto wangu,” alisema Bi Joyce Naeni, mkazi wa eneo la Father Ntaiyia.

Katika kisa cha pili, mwili wa naibu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Lengesurai George Olonana ulipatikana ukining'inia kwenye mti ukiwa na kamba ya mkonge shingoni katika eneo la Olchorro katika Kaunti Ndogo ya Narok Kaskazini.

Mwili wa Olonana, 34, haukuwa na majeraha yaliyoonekana lakini marehemu alikuwa ameacha barua ya kujitoa mhanga akiwaomba walimu wenzake na familia kumsamehe kwa hatua aliyochukua.

Miili hiyo miwili ilihamishiwa kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok kwa uhifadhi ikisubiri uchunguzi wa maiti.

Kufuatia visa hivyo, mkuu wa polisi kaunti hiyo ametoa wito kwa watu wanaougua msongo wa mawazo kutafuta mwongozo na ushauri kutoka kwa jamaa wa karibu au viongozi wa kidini ambao wanaweza kuwatia moyo.

Kamanda huyo aliwakumbusha kuwa kujiua hakutatui tatizo lolote, huku akizingatia kuwa kila changamoto wanayokumbana nayo maishani ina suluhu iwapo itashughulikiwa ipasavyo.

(Samuel Maina)