Wakili auawa kwa kudungwa kisu Ongata Rongai

Muhtasari

• Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kimetoa wito kwa idara husika kumtafuta mtu aliyemuua Nyakeri Jumamosi asubuhi.

• Wawili hao walikuwa wamemwona mwanamume huyo akiwafuata lakini kabla hawajaamua kumkabili ama kukimbia ili kujinusuru alimshambulia Nyakeri kwa kumdunga kisu shingoni.

• Binamuye alijaribu kumuokoa na pia akashambuliwa kwa kisu na jamaa huyo aliyekuwa pekee yake kabla ya kutoroka.

Wakili Boaz Nyakeri
Wakili Boaz Nyakeri
Image: HISANI

Polisi wanachunguza kisa cha mauaji ya wakili Boaz Nyakeri aliyedungwa kisu alipokuwa akielekea nyumbani katika eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado.

Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kimetoa wito kwa idara husika kumtafuta mtu aliyemuua Nyakeri Jumamosi asubuhi.

Nyakeri alidungwa kisu shingoni karibu na eneo Masaai Lodge katika viunga vya Ongata Rongai.

Binamu yake ambaye alikuwa naye wakati wa shambulio hilo pia alidungwa kisu na kujeruhiwa kwenye mkono alipokuwa akijaribu kumwokoa marehemu.

Sababu ya shambulio hilo bado haijajulikana, polisi na familia walisema.

Polisi walisema uchunguzi wa awali waonyesha kuwa Nyakeri na binamu yake walikuwa wakitoka kwenye hafla karibu na Osoita Lodge na walikuwa wakirejea nyumbani mwendo wa saa tano usiku wa Jumamosi wakati mwanamume mmoja alipowashambulia.

Wawili hao walikuwa wamemwona mwanamume huyo akiwafuata lakini kabla hawajaamua kumkabili ama kukimbia ili kujinusuru alimshambulia Nyakeri kwa kumdunga kisu shingoni.

Binamuye alijaribu kumuokoa na pia akashambuliwa kwa kisu na jamaa huyo aliyekuwa pekee yake kabla ya kutoroka.

Polisi walisema msamaria mwema alimkimbiza katika Hospitali ya Sinai ambako alipewa rufaa ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta lakini alifariki alipokuwa akihudumiwa.

Alikuwa amevuja damu nyingi. Mwili wake unahifadhiwa katika chumba ya cha maiti huku upasuaji wa maiti ukitarajiwa kufanyika siku ya Jumatano.

Binamuye marehemu alihudumiwa hospitalini na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Alisomea Shahada ya Sheria (LLB) katika Chuo Kikuu cha Africa Nazarene na amekuwa akifanya kazi katika kampuni ya kisheria.

Afisa Mkuu Mtendaji wa LSK Mercy Wambua alikashifu shambulizi hilo akisema jukumu lililowekwa kwa mawakili kama maafisa wa mahakama na watetezi wa haki za binadamu linawaweka katika hatari kubwa zaidi ya uwezekano wa kushambuliwa na wanaohisi kudhulumiwa.

 “Ni kutokana na hali hiyo tunaiomba Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha mawakili, mahakimu, pamoja na wahudumu wote wa mahakama wanapewa ulinzi wa kutosha dhidi ya aina yoyote ya madhara, vitisho na mashambulizi ambayo yanaweza kutokea kutokana na kazi zao,” alisema.

Aliomba mamlaka kuimarisha vyombo vya usalama nchini, hasa katika msimu wa sikukuu.

Maafisa wa upelelezi kutoka Ongata Rongai DCI walizuru eneo la tukio Jumamosi kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo.

Walisema hakuna mtu aliyekamatwa na kwamba msako wa mshambuliaji unaendelea.