Wanandoa wauawa, binti yao kujeruhiwa baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kujilipua Kisumu

Mshambuliaji pia alikufa papo hapo.

Muhtasari

•Duru za kuaminika  zilisema mshambuliaji ni mtu aliyerejea kutoka kwa kundi la kigaidi la Alshaabab.

•Miaka miwili iliyopita mshambuliaji alijaribu kuua mpenzi wake wa miaka 16 ndania ya nyumba ya kupanga katika mji wa Katito kwa madai ya kutokuwa mwaminifu katika mahusiano.

Kilipuzi kilichotengenezwa kienyeji
Kilipuzi kilichotengenezwa kienyeji
Image: MAKTABA

Watu watatu wamefariki baada ya mshambuliaji wa kujitolea mhanga kujilipua katika eneo la Nyakach, kaunti ya Kisumu.

Wahasiriwa ambao ni mume na mke wenye umri wa miaka 55 waliangamia kufuatia mlipuko huo ambao ulitokea Jumanne mwendo wa saa kumi na moja jioni. 

Mwanamke alifariki papo hapo huku mumewe akiaga alipokuwa anapokea matibabu hospitalini moja mjini Kisumu. Mshambuliaji pia alikufa papo hapo.

Binti ya wahasiriwa alinusurika na majeraha na amelazwa hospitalini ambako anaendelea kuhudumiwa.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la ndani lililo kwenye mpaka wa kaunti za Kisumu na Kericho.

Duru za kuaminika  zilisema mshambuliaji ni mtu aliyerejea kutoka kwa kundi la kigaidi la Alshaabab ambaye alitumia kilipuzi kilichotengenezwa kienyeji alichokuwa amekifunga kiunoni.

Inadaiwa kwamba miaka miwili iliyopita mshambuliaji alijaribu kuua mpenzi wake wa miaka 16 ndania ya nyumba ya kupanga katika mji wa Katito kwa madai ya kutokuwa mwaminifu katika mahusiano.

Mshambuliaji alishuku mpenzi wake alikuwa anatongozwa na wanaume wenginena hapo ndipo akafanya jaribio la kumuua kutumia kilipuzi.

Kulingana na polisi, mhasiriwa alitengeneza kilipuzi na kuacha ndani ya nyumba ambayo mpenzi wake alikuwa na baadae kilipolipuka kikasababishia mwanadada yule majeraha.

Mshambuliaji ambaye ni yatima aliyeacha shule akiwa katika darasa la tano anaripotiwa kutoka nyumbani miaka mitano iliyopita kuelekea Mombasa ambako alijiunga na kundi la Alshabaab kisha kurejea baadae.

Polisi walisema mshambuliaji alifanya kazi katika mgodi wa kokoto kabla ya kujiunga na Alshabaab.

Raia wameagizwa kukaa macho na kuripoti shughuli za kushukiwa katika vituo vya polisi vilivyo karibu huku polisi wakisema wameboresha usalama kufuatia tukio hilo.