Mwanafunzi aliyeteketeza bweni la Moi Girls na kusababisha vifo 10 apatikana na hatia ya kuua bila kukusudia

Muhtasari

•Alipokuwa anamtia hatiani, Hakimu Stella Mutuku alisema mshtakiwa hakuwasha moto huo akiwa na nia ya kuwaua wenzake bali ni kitendo kilichotokana na jaribio lake la kutaka ahamishwe kutoka shule hiyo kwa njia yoyote ile.

Lango la shule ya upilii ya Moi Girls
Lango la shule ya upilii ya Moi Girls
Image: MAKTABA

Mwanafunzi aliyewasha moto ambao ulisababisha vifo vya wenzake 10 katika shule ya upili ya wasichana ya Moi, jijini Nairobi mnamo 2017 amepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia.

Mshtakiwa alikuwa na umri wa miaka 14 wakati tukio hilo lilitokea. Alikuwa analala katika bweni la bweni la Kabarnet ambapo moto huo ulizuka.

Alipokuwa anamtia hatiani, Hakimu Stella Mutuku alisema mshtakiwa hakuwasha moto huo akiwa na nia ya kuwaua wenzake bali ni kitendo kilichotokana na jaribio lake la kutaka ahamishwe kutoka shule hiyo kwa njia yoyote ile.

"Huenda lengo lake lilikuwa ni kuwasha moto na kuteketeza jengo bila kumuumiza mtu yeyote lakini ilikuwa ni jambo mbaya kwa  kuwa jengo hilo lilikuwa na ghorofa mbili na moto huo ungesababisha vifo" Mutuku alisema.

Hakimu alisema huenda mshtakiwa alipuuza matokeo ya matendo yake. Jaribio lake la kuwaamsha baadhi ya marafiki zake lilikuwa na lengo la kuwaokoa kutoka kwenye moto.

Katika hukumu yake, Mutuku alisema hawezi kumpata mshukiwa na kosa la mauaji kwa kuwa mwendesha mashitaka alishindwa kuthibitisha kiini cha uovu uliofikiriwa hapo awali.

Hakimu hakumpata mshtakiwa na kosa la mauaji katika makosa yote 10 yanayomkabili.

"Anaachiliwa katika makosa kumi ya mauaji yanayomkabili. Badala yake, naona kosa hilo limethibitishwa pasipo shaka kuwa ni kuua bila kukusudia katika makosa yote 10," Hakimu alisema.

Mahakama ilimpata na hatia ya kuua bila kukusudia.

Mnamo tarehe 1 Septemba 2017, bweni la Kabarnet liliteketezwa kwa moto mkali uliosababisha vifo vya wanafunzi 10 ambao walikuwa wametoka tu kuripoti shuleni na familia zao zikaomboleza kwa kuwapoteza binti zao.

Mshtakiwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 14 na aliishi katika bweni la Kabarnet. Sasa ana miaka 18.