COVID 19: Visa vipya 1, 596 vyaripotiwa; 19, 620 wanapokea matibabu

Wagonjwa 330 wameweza kupata afueni

Muhtasari

•Wizara ya afya imeripoti vifo vipya vitatu kutokana na ugonjwa huo. Idadi ya walioangamia kufikia sasa ni 5, 364.

•Watu 5, 639, 933 wameweza kupokea angalau dozi moja ya chanjo huku 3, 939, 523 kati yao wakiwa wamepokea dozi zote mbili.

Waziri Mutahi Kagwe
Waziri Mutahi Kagwe
Image: MOH

Kiwango cha maambukizi ya virusi vya Corona imefikia 37.6% huku visa vipya 1,596 vikiripotiwa kutoka kwa sampuli 4, 242 ambazo zimepimwa katika kipindi cha masaa 24 ambacho kimepita.

Idadi hiyo mpya imefikisha jumla ya maambukizi nchini kuwa 284, 150 kutoka kwa sampuli 2, 999, 912 ambazo zimepimwa.

Mtoto wa miezi minane na mkongwe wa miaka 91 ni miongoni mwa wagonjwa wapya wa COVID 19. 

Kaunti ya Nairobi inaendelea kuongoza kwa maambukizi huku ikiripoti visa vipya 683, Siaya inafuata na visa 213, Muranga ya tatu na visa 133 huku kaunti zingine zikiripoti visa chini ya 100.

Wagonjwa 330 wameweza kupata afueni, 196 kati yao ambao walikuwa wamelazwa hospitalini huku 134 wakiponea manyumbani kwao.

Wizara ya afya imeripoti vifo vipya vitatu kutokana na ugonjwa huo. Idadi ya walioangamia kufikia sasa ni 5, 364.

Wagonjwa 708 wamelazwa katika vituo mbalimbali vya afya huku wengine 19, 315 wakiendelea kupokea matibabu nyumbani. Wagonjwa 31 wamelazwa katika ICU.

Chanjo ya Corona

Kufikia sasa jumla ya chanjo 9, 579, 456 zimepeanwa. 

Watu 5, 639, 933 wameweza kupokea angalau dozi moja ya chanjo huku 3, 939, 523 kati yao wakiwa wamepokea dozi zote mbili.