Raila Odinga ampiku Ruto kama mgombeaji maarufu zaidi wa urais katika utafiti mpya

Muhtasari

•Utafiti huo ambao ulifanywa kati ya Septemba 17 na Desemba 21, ulisema umaarufu wa Raila ulifikia asilimia 33 huku ule wa Ruto ukiwa asilimia 32.

•Cha kushangaza  ni kwamba, Wakenya wengi (asilimia 52) wanataka Muungano wa Umoja wa Kenya (Oka) kuvunjwa na viongozi wake kujiunga na aidha Raila au Ruto.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga
Kiongozi wa ODM Raila Odinga
Image: MAKTABA

Kinara wa ODM Raila Odinga angenyakua kiti cha urais na kumshinda naibu rais William Ruto kwa kura ndogo iwapo uchaguzi ungefanyika leo, kura ya maoni imebaini.

Kura ya maoni ya Infotrak Voice of the People, ambayo ilikusanya maoni ya Wakenya kuhusu uchaguzi wa urais mwaka ujao, ilisema kinyang'anyiro hicho kitakuwa mbio za hapa kwa hapa kati ya farasi wawili.

Utafiti huo ambao ulifanywa kati ya Septemba 17 na Desemba 21, ulisema umaarufu wa Raila ulifikia asilimia 33 huku ule wa Ruto ukiwa asilimia 32.

Infotrak ulifanya mahojiano hayo kupitia  mahojiano ya simu kwa usaidizi wa Kompyuta (CATI)

Utafiti w ulilenga na sampuli ya wahojiwa 1,600 ambao walikuwa na umri wa miaka 18 na zaidi wakati wa mahojiano.  Upeo wa hitilafu ulikuwa wa kuongeza au kupunguza asilimia 2.45.

Kura ya maoni ilionyesha umaarufu wa Ruto umekuwa ukishuka hatua kwa hatua katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho kimepita huku ule wa Raila ukiimarika haswa baada ya Kongamano la mwisho la Azimio La Umoja mnamo tarehe 10 Disemba 2021 ambapo alitangaza kuwania urais.

Utafiti huo ulisema umaarufu wa Ruto mnamo Desemba mwaka jana ulikuwa asilimia 44, ukapungua hadi asilimia 34 mnamo Novemba 2021 na kisha asilimia 32 mnamo Desemba 2021.

Kwa upande mwingine umaarufu wa Raila ulikuwa asilimia 13 mnamo Desemba 2020, ukapanda hadi asilimia 25 mnamo Novemba 2021 na kupanda hadi asilimia 33 baada ya hafla ya Azimio katika Kituo cha Michezo cha Kimataifa cha Moi Kasarani.

Umaarufu wa Musalia Mudavadi (ANC) na Kalonzo Musyoka (Wiper) wote ulisimama kwa asilimia moja kila mmoja.

Hata hivyo, asilimia kubwa ya Wakenya bado hawajafanya maamuzi kwani asilimia 21 bado hawajaamua.

Chama cha Ruto cha UDA hata hivyo ndicho kilikuwa maarufu zaidi kwa asilimia 33 kikifuatiwa na ODM kwa asilimia 32 huku Wiper, Kanu, Ford Kenya na vingine vikichukua asilimia 35.

Cha kushangaza  ni kwamba, Wakenya wengi (asilimia 52) wanataka Muungano wa Umoja wa Kenya (Oka) kuvunjwa na viongozi wake kujiunga na aidha Raila au Ruto.

Asilimia 55 ya wanaotaka Oka avunjiliwe mbali wanataka vinara wa muungano huo (Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetang'ula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu) kumuunga mkono Raila.

Asilimia 44 ya waliohojiwa wanataka Mudavadi awe mgombea mwenza wa Ruto au Raila,  asilimia 19 wanataka Kalonzo awe mgombea mwenza huku asilimia 11 wakipendekeza Moi na Wetang'ula (asilimia 3).

Asilimia ishirini na moja hawakutoa mapendekezo yoyote.

Kura hiyo ilitaja maeneo ya Kati, Bonde la Ufa, Mashariki na Nairobi kuwa ngome za Ruto huku Raila akiungwa mkono Magharibi, Pwani, Nyanza na Kaskazini Mashariki.