Jamaa ajitia kitanzi baada ya pikipiki yake kuibwa Mwingi

Muhtasari

•Nicholas Nzau 23, alijitia kitanzi akiwa ndani ya bafu la nyumba yake ya kukodi mnamo Jumatatu jioni.

•Kaka ya marehemu, Francis Muthiani, alisema kakake alikuwa na msongo wa mawazo baada ya pikipiki yake kuibiwa

Image: HISANI

Jamaa mmoja kutoka mji wa Mwingi, Kaunti ya Kitui amejitia kitanzi kwa kile kinachoaminika kuwa msongo wa mawazo uliosababishwa na wizi wa pikipiki yake.

Nicholas Nzau 23, alijitia kitanzi akiwa ndani ya bafu la nyumba yake ya kukodi mnamo Jumatatu jioni.

Mke wake Ruth Mwikali alisema alimuacha na binti yao wa miezi minne na kwenda kazini. Aliporejea nyumbani alipata mlango wa nyumba yao ukiwa umefungwa upande wa ndani.

Juhudi za kuwasiliana na mumewe kwa simu hazikufua dafu kwani simu yake ilikereza ila hakuna aliyepokea.

Ruth alizunguka sehemu kadhaa ambapo alidhani mumewe angekuwa ila hakufanikiwa kumpata. Hapo ndipo akaamua kuvunja mlango na kugundua Nzau alikuwa amejitia kitanzi.

Mtoto wao alikuwa amelala kitandani huku akiwa analia.

"Pikipiki ya mume wangu iliibiwa mwezi mmoja uliopita na amekuwa na msongo wa mawazo kwani ilikuwa inamsaidia katika biashara yake ya uchuuzi. Aliacha kwenda kazini, aliitumia kuzungusha vitu vya jua kali. Nilikuwa nikimwacha na binti yetu ili kumfanya awe busy na kusahau misukosuko aliyokuwa akipitia," Ruth alisimulia.

Inasemekana Nzau alinunua pikipiki hiyo kwa Ksh.140,000 na hakuweza kukubali kwamba ilikuwa imetoweka.

"Nilikuwa nikimtia moyo asiwe na wasiwasi kwani angeweza kuinuka tena kiuchumi kwa sababu alikuwa mtu mchapakazi sana," Ruth aliongeza.

Baada ya kupata mwili wa mumewe, Ruth aliwaarifu majirani, familia ya marehemu na kuenda katika kituo cha polisi cha Mwingi kupiga ripoti.

Kaka ya marehemu, Francis Muthiani, alisema kakake alikuwa na msongo wa mawazo baada ya pikipiki yake kuibwa.

"Tulizungumza Jumatatu saa 12 jioni akaniambia anataka kulala kwa vile alikuwa akikosa usingizi usiku. Aliahidi kunipigia jioni ila nikapokea taarifa za kifo chake cha ghafla kutoka kwa mkewe," Alisema.

Marehemu ameacha mke na watoto wawili. Mkubwa ana umri wa miaka 3.

Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mwingi Level 4 na maafisa wa polisi.