Jamaa apigwa kitutu baada ya kunaswa akijaribu kubaka mwanamke Kiambu

Muhtasari

•Katika juhudi za kutosheleza kiu chake cha tendo la kitandani, Kariuki anaripotiwa kumvizia mhasiriwa katika eneo iliyojificha alipokuwa akirejea nyumbani kwake katika kijiji cha Nyaga kutoka madukani ya Kwa Maiko.

crime scene 1
crime scene 1
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ya Kiambu wanamzuilia jamaa mmoja mwenye umri wa miaka 38 kwa kujaribu kubaka mwanamke katika eneo la Githunguri.

Peter Kariuki alinusurika kifo baada ya polisi kumuokoa kutoka kwa umati wa watu wenye ghadhabu ambao walitaka kumfunya kuwa funzo kwa wahalifu wengine walipomnasa akiwa karibu kufanya kitendo hicho cha aibu.

Katika juhudi za kutosheleza kiu chake cha tendo la kitandani, Kariuki anaripotiwa kumvizia mhasiriwa katika eneo iliyojificha alipokuwa akirejea nyumbani kwake katika kijiji cha Nyaga kutoka madukani ya Kwa Maiko.

Kulingana na DCI, mhasiriwa hakumpa mshukiwa nafasi ya kumdhulumu na akapambana naye akiwa amelala huku akipiga kelele iliyowavutia wapita njia ambao walikimbia pale na kumuokoa.

Baada ya kumuokoa mwanamke yule kutoka mikononi mwa mshukiwa, umati ule ulimgeukia Kariuki na kumshambulia kwa ngumi, mateke na makofi wakitaka kumfunza adabu aliyokosa.

Kuwasili kwa maafisa kutoka kituo cha polisi cha Ngewa katika eneo la tukio kulipatia mshukiwa nafasi nyingine ya kuishi kwani walitawanya umati wa watu waliokuwa wanamshambulia.

Polisi walipomkagua mshukiwa walipata simu ya mhasiriwa ambayo alikuwa ameiba na kutia mfukoni tayari.

Kariuki alikimbizwa katika kituo cha afya cha Ngewa ambako alihudumiwa kabla ya kutiwa pingu na kuwekwa kizuizini.