Polisi akamatwa akijaribu kuuza bunduki yake mjini Naivasha

Muhtasari

•Afisa huyo  alikuwa amefika katika klabu moja mjini Naivasha pamoja na watu wengine wawili tayari kuuza bastola yake ya ceska ikiwa na risasi 40.

•Haijabainika polisi huyo alitaka kuuza bastola yake ambayo alikabidhiwa na serikali kwa kiasi gani cha pesa. 

Picha ya bastola aina ya Ceska
Picha ya bastola aina ya Ceska
Image: MUSEMBI NZENGU

Polisi mmoja alitiwa mbaroni siku ya Jumanne alipokuwa anajaribu kuuza bunduki katika mji wa Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Afisa huyo  alikuwa amefika katika klabu moja mjini Naivasha pamoja na watu wengine wawili tayari kuuza bastola yake ya ceska ikiwa na risasi 40.

Kando na risasi 15 zilizokuwa kwenye bastola hiyo, mshukiwa alikuwa na risasi zingine 25 kwenye kijisanduku, jambo ambalo liliashiria alitaka kuziuza.

Haijabainika polisi huyo alitaka kuuza bastola yake ambayo alikabidhiwa na serikali kwa kiasi gani cha pesa. 

Konstebo Patrick Kimani ambaye anahudumu katika makao makuu ya polisi lakini na pia  katika  Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) alikamatwa baada ya kueleka klabuni tayari kufanya biashara.

Inadaiwa alikuwa ameomba mtu mmoja pale mjini Naivasha amtafutie mnunuzi wa bunduki aliyokuwa nayo.Hapo ndipo polisi walipopata taarifa wakajifanya wanunuzi na kuanzisha tovuti kwa ajili ya biashara hiyo.

Polisi walisema walifanikiwa kupata bastola kutoka kwa watatu hao pamoja na gari walilokuwa wanatumia.  Washukiwa hao waliwekwa kizuizini na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Mkuu wa polisi katika eneo la Bonde la Ufa Fredrick Ochieng alisema wanachunguza kubaini iwapo kuna wengine waliohusika.

"Hatuwezi kubaliana na mambo kama haya na ndiyo maana yanapelekwa mahakamani,” alisema.

Suala hilo linachafua zaidi taswira ya idara ya polisi. Idara ya Kitaifa ya Polisi inajitahidi kuondoa taswira mbaya ya kuhusika katika uhalifu mwingi.