Watu 6 wafa maji katika kipindi cha siku nne Machakos

Muhtasari

•Kulingana na Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Mwala (ACC) Damaris Mutanu watatu kati ya waathiriwa walikufa maji katika matukio matatu tofauti siku ya Jumatano.

•Usiku wa Krismasi, Joshua Kula mwenye umri wa miaka 30 alisombwa na maji mazito pamoja na gari lake mtoni Mithini karibu na mji wa Masii mwendo wa saa 9.30 jioni.

Mto Sabaki huko Magarini, kaunti ya Kiifi, Aprili 24, 2020.
Mto Sabaki huko Magarini, kaunti ya Kiifi, Aprili 24, 2020.
Image: ALPHONCE GARI

Watu sita akiwemo msichana wa miaka 11 wamekufa maji katika eneo la Mwala, kaunti ya Machakos katika kipindi cha  siku nne ambacho kimepita.

Kulingana na Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Mwala (ACC) Damaris Mutanu watatu kati ya waathiriwa walikufa maji katika matukio matatu tofauti siku ya Jumatano.

 Katika tukio la kwanza, mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu alikufa maji alasiri alipokuwa akijaribu kuvuka mto Kyaimu eneo la Miu.

Katika tukio la pili, mwili wa Teresia Mbithe, ulipatikana ukielea kwenye bwawa moja la maji katika kijiji cha Mutuyu mida ya saa nane asubuhi.

Mutanu alisema Mbithe aliripotiwa kutoweka na familia yake mwendo wa saa kumi jioni ya Jumanne.

Katika tukio la tatu, mwili wa mtu ambaye hajafahamika jina lake ulipatikana ukiwa umezikwa na mchanga kwenye mto Munzu katika eneo la Mbiuni.

Mwanamume huyo anashukiwa kufa maji Jumanne usiku alipokuwa anavuka mto.

Siku ya Jumatatu mwili mwingine wa mtu ambaye hajafahamika jina uligunduliwa kwenye kingo za mto Thwake katika kijiji cha Ikotheni, eneo ndogo la Kilala.

Siku ya Boxing Day, Muli Thathi mwenye umri wa miaka 32 alizama kwenye mto Miu, katika tarafa ya Yathui alipokuwa akijaribu kumsaidia rafiki yake kuvuka mto uliofurika. Walikuwa wamelewa tukio hilo lilipotokea. Mwili wake bado haujapatikana.

Usiku wa Krismasi, Joshua Kula mwenye umri wa miaka 30 alisombwa na maji mazito pamoja na gari lake mtoni Mithini karibu na mji wa Masii mwendo wa saa 9.30 jioni.

Kula alikuwa akiendesha gari kuelekea nyumbani kutoka kwa mapumziko ya karibu akiandamana na rafiki wakati kisa hicho kilipotokea.

Rafiki huyo hata hivyo aliweza kuogelea hadi eneo salama. Mwili wake ulipatikana Jumanne baada ya msako wa siku mbili huku gari hilo likitolewa karibu mita 200 kutoka eneo la tukio.

ACC ametoa tahadhari kutokana na matukio ya kuzama kwa maji na kuwataka wakazi kuacha kuvuka mito iliyofurika.

“Natoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuwa na subira, wanapopata maji yanayochafuka, wasubiri hadi viwango vishuke badala ya kuhatarisha maisha yao,” alisema.

Mutanu aidha amewataka wakaazi wenye madimbwi ya shamba na vibandiko vya maji kuyalinda ili kuzuia watoto kuzama. "Wazazi wanapaswa kuwa waangalifu na kuhakikisha kwamba watoto hawaishii kuzama kwenye vyanzo hivyo vya maji majumbani," aliongeza.

(Utafsiri: Samuel Maina)