Wanafunzi wapenzi wa jinsia moja kupigwa marufuku kujiunga na shule za bweni

Muhtasari

•Magoha amesema badala yake wanafunzi hao wanapaswa kuhudhuria shule za kutwa zilizo karibu na makazi yao.

•Mapenzi ya jinsia moja hapa nchini yanaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha jela cha hadi miaka 14.

Waziri wa Elimu George Magoha
Waziri wa Elimu George Magoha
Image: MAKTABA

Waziri wa elimu Prof George Magoha ameagiza wanafunzi wote ambao ni wapenzi wa jinsia moja wasiruhusiwe kuhudhuria shule za bweni. 

Magoha amesema badala yake wanafunzi hao wanapaswa kuhudhuria shule za kutwa zilizo karibu na makazi yao.

Kulingana na Magoha, iwapo wanafunzi wanaovutiwa kimapenzi na wenzao wa jinsia wataruhusiwa katika shule za bweni huenda wakawashawishi  wanafunzi wengine kujiunga nao.

Magoha amependekeza kwamba wanafunzi kama wale ambao tayari wako katika shule za bweni wanapaswa kuhamishwa na kupelekwa katika shule za kutwa.

“Wajibu wako unapaswa kuwa kwa walio wengi zaidi na sio watu wachache. Usijiruhusu kutishwa na watoto” Magoha aliwaagiza walimu wakuu.

Suala hili limeibua gumzo moto huku mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yakiapa kufika mahakamani kupinga utekelezaji wa agizo la waziri huyo.

Baadhi ya wanamitandao wamemuunga mkono waziri huku wengine wakimkashifu  kwa kile wanachosema ni  maoni ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wa LGBT.

Mapenzi ya jinsia moja hapa nchini yanaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha jela cha hadi miaka 14.