Gavana Mutua aomba msamaha kwa kuchapisha habari za uongo kuhusu kifo cha mke wa Kalonzo

Muhtasari

•Mgombeaji huyo wa kiti cha urais katika chaguzi za mwezi Agosti amesema alipotoshwa na watu kadhaa walio karibu sana na Kalonzo.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua wakati wa uzinduzi wa manifesto yake ya Urais katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Desemba 5, 2021.
Gavana wa Machakos Alfred Mutua wakati wa uzinduzi wa manifesto yake ya Urais katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Desemba 5, 2021.
Image: ISAIAH LANGAT

Gavana wa Machakos Alfred Mutua ameomba radhi kufuatia habari za uwongo alizochapisha hapo awali kuhusu kifo cha mke wa kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Mgombeaji huyo wa kiti cha urais katika chaguzi za mwezi Agosti amesema alipotoshwa na watu kadhaa walio karibu sana na Kalonzo.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mutua  amesema habari alizopewa kuhusu hali ilivyo katika familia ya Kalonzo zilionekana kuwa za kweli.

"Ningependa kuomba radhi kwa chapisho la awali kuhusu familia ya H.E. Kalonzo Musyoka. Haya yalitokana na taarifa potofu na ulaghai kutoka kwa watu kadhaa, wengine, wakionekana kuwa wa kuaminika na wa karibu na H.E. Kalonzo, ambao walifanya ionekane kama ujumbe kwangu kuhusu familia yake" Mutua amesema.

Gavana huyo ameomba radhi kwa kusababisha wasiwasi huku akilaani waliompatia habari hizo potofu.

Hapo awali Mutua  alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kufariji familia ya Kalonzo kufuatia 'kifo' cha Bi Pauline Kalonzo, jumbe ambazo alifuta dakika chacha baadae kabla ya kuomba msamaha. 

Mutua alikuwa amemwomboleza Mama Pauline kama mwanamke mtulivu na aliye na sifa nzuri za mama.

Ujumbe ambao Mutua alichapiha kabla ya kuufuta na kuomba msamaha
Ujumbe ambao Mutua alichapiha kabla ya kuufuta na kuomba msamaha
Image: SCREENSHOT

Mapema siku ya Jumapili kupitia Citizen TV Kalonzo alikuwa ametoa taarifa kuhusu hali ya afya ya mkewe akisema kwamba anaendelea kupokea matibabu na afya yake iko imara.