Watu 8 wafariki baada ya matatu iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi kugonga lori Kakamega

Hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Musembe.

Muhtasari

•Inasemekana matatu hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Webuye  ilikuwa imebeba watu wanane wakati wa ajali.

•Dereva wa lori alisema alikuwa amesimama nyuma ya trela nyingine iliyokuwa imeharibika ili kumsaidia dereva wakati Nissan iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi iligonga lori lake kwa nyuma

Inasemekana matatu hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Webuye ilikuwa imebeba watu wanane wakati wa ajali.
Inasemekana matatu hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Webuye  ilikuwa imebeba watu wanane wakati wa ajali.
Image: HILTON OENYO

Watu wanane walifariki papo hapo baada ya matatu waliyokuwa wakisafiria kugonga lori moja katika barabara kuu ya Webuye-Eldoret alfajiri ya Jumapili.

Hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Musembe.

Kamanda wa polisi katika eneo la Magharibi Perris Kimani alithibitisha tukio hilo.

"Ni kama dereva aliingiwa na hofu baada ya kuona lori lililosimama ghafla na kujaribu kukwepa lakini lori hilo lilipasua paa ya matatu na vyuma vikakata vichwa watu wote waliokuwamo," Kimani alisema.

Inasemekana matatu hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Webuye  ilikuwa imebeba watu wanane wakati wa ajali.

Miili ya walioangamia  ilipelekwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ndogo ya Webuye, ikisubiri uchunguzi wa maiti.

Dereva wa lori ambalo matatu hiyo iligonga, Nicholas Mwangi alisema alikuwa amesimama nyuma ya trela nyingine iliyokuwa imeharibikia kando ya barabara ili kumsaidia dereva wakati Nissan iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi iligonga lori lake kwa nyuma.

“Niliona lori mbele ambalo dereva wake namfahamu alikuwa amekwama barabarani hivyo nikapunguza mwendo na kusimama nyuma yake. Lakini muda mfupi baada ya kushuka nilisikia kishindo na kuona paa ya matatu ikipasuka,” Mwangi alisema.

Mwangi alikuwa anasafiri kutoka Uganda kuelekea Eldoret.

Bado haijafahamika iwapo waliofariki walikuwa wanafamilia au abiria waliochanganyika.

Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama, zaidi ya watu 3,500 walipoteza maisha barabarani kati ya Januari na Novemba, 2021.

Mamlaka imesema kati ya vifo 3,564 vilivyosajiliwa, watembea kwa miguu na waendesha pikipiki ndio walioathirika zaidi na vifo 1,241 na 984, mtawalia.

Mnamo Desemba 2021, NTSA ilizindua mipango kadhaa ya usalama barabarani ili kuwahamasisha watumiaji wa barabara huku wakipanga kusafiri hadi maeneo mbalimbali kwa sherehe za Krismasi.

(Utafsiri: Samuel Maina)