Timu ya Kalonzo yalaani habari za uongo zilizodai kwamba mkewe ameaga

Muhtasari

•Mkuu wa mawasiliano katika SKM Command Center Paloma Gatabaki alipuuzilia mbali uvumi uliokuwa unaenezwa mitandaoni siku ya Jumapili kwamba bi Pauline alikuwa ameaga dunia.

Kalonzo Musyoka katika studio za Radio Jambo mnamo tarehe 1 mwezi Septemba
Kalonzo Musyoka katika studio za Radio Jambo mnamo tarehe 1 mwezi Septemba
Image: ANDREW KASUKU

Bi Pauline Kalonzo ambaye ni mke wa kiongozi wa Wiper Stephen Kalonzo Musyoka yuko hai, timu ya kampeni ya makamu huyo wa rais wa zamani imethibitisha.

Kupitia kwa ujumbe uliotolewa kwa wanahabari,  mkuu wa mawasiliano katika SKM Command Center Paloma Gatabaki alipuuzilia mbali uvumi uliokuwa unaenezwa mitandaoni siku ya Jumapili kwamba bi Pauline alikuwa ameaga dunia.

Gatabaki alisema habari zilizokuwa zinaenezwa haswa kwenye mtandao wa Twitter si za kweli huku  akilaani kitendo hicho cha kuchukiza 

"Hizo ni habari za uongo. Inasikitisha kuona tunaishi nyakati ambapo watu wanatumia muda wao wakijaribu kupata 'clicks' na kutosema ukweli. Inahuzunisha kuwa wanaoeneza habari hizo za chuki, za kutisha na za uwongo hawajaonyesha majuto kwa uharibifu wanaosababisha" Gatabaki alisema.

Timu hiyo pia imewaonya Wakenya dhidi ya kuendelea na tabia kama ile.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua ni mmoja wa walioanguka kwa mtego wa kusambaza habari za uongo kuhusu kifo cha Bi Pauline.

Mutua  alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kufariji familia ya Kalonzo kufuatia 'kifo' cha Bi Pauline Kalonzo, jumbe ambazo alifuta dakika chacha baadae kabla ya kuomba msamaha. 

Mutua alikuwa amemwomboleza Mama Pauline kama mwanamke mtulivu na aliye na sifa nzuri za mama.

Baadae mgombeaji huyo wa kiti cha urais katika chaguzi za mwezi Agosti alisema alipotoshwa na watu kadhaa walio karibu sana na Kalonzo.

"Ningependa kuomba radhi kwa chapisho la awali kuhusu familia ya H.E. Kalonzo Musyoka. Haya yalitokana na taarifa potofu na ulaghai kutoka kwa watu kadhaa, wengine, wakionekana kuwa wa kuaminika na wa karibu na H.E. Kalonzo, ambao walifanya ionekane kama ujumbe kwangu kuhusu familia yake" Mutua alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.