Seneta Malala amjibu Raila baada yake kumbatiza jina 'Omondi'

Muhtasari

•Malala alisema anajivunia majina ambayo Raila anambandika huku akidai kuwa anaamini yatamsaidia kunyakua kura nyingi kutoka kwa jamii husika na kutwaa kiti cha urais hata kabla yake.

Seneta Cleopas Malala
Seneta Cleopas Malala
Image: MAKTABA

Senata wa Kakamega Cleophas Malala Wakhungu amemjibu kinara wa ODM Raila Odinga baada yake kumbandika jina 'Omondi'.

Alipokuwa anahutubia wakazi wa Kakamega mapema wiki hii, Malala alisema amekubali jina alilopewa na waziri huyo mkuu wa zamani na kulitaja kama jina la baraka.

Malala alisema anajivunia majina ambayo Raila anambandika huku akidai kuwa anaamini yatamsaidia kunyakua kura nyingi kutoka kwa jamii husika na kutwaa kiti cha urais hata kabla yake.

"Mimi kama kiongozi wa taifa nitakubali majina yote. Nitakubali jina Omondi ambalo Raila amenipa, Wakikuyu watanipatia Karanja, Wamasai watanipatia la Ole Kina, Wakamba watanipatia ya Musyoka. Hizo majina unanipatia Raila zitanifanya niwe rais wa Kenya kabla yako. Nimekubali Baba Raila asante sana kwa kunipatia jina Omondi. Hiyo ni baraka, ile siku nitasimama urais niko na uhakika jamii ya dholuo yote itapigia Malala Omondi kura" Malal alisema.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita wakati Raila alipokuwa anahutubia umati uliokuwa umejumuika katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega alidai kwamba Malala ana asili ya jamii ya Dholuo.

Raila alisema babu ya  Malala alizikwa katika eneo la Ugenya, kaunti ya Siaya ambako alidai ndiko nyumbani halisi kwa kina Malala.